Ufunuo 7:1-12
Ufunuo 7:1-12 SRUV
Baada ya hayo nikaona malaika wanne wamesimama katika pembe nne za nchi, wakizizuia pepo nne za nchi, upepo usivume juu ya nchi, wala juu ya bahari, wala juu ya mti wowote. Nikaona malaika mwingine, akipanda kutoka maawio ya jua, akiwa na mhuri wa Mungu aliye hai; akawaita kwa sauti kuu wale malaika wanne waliopewa kuidhuru nchi na bahari, akisema, Msiidhuru nchi, wala bahari, wala miti, hadi tutakapokwisha kuwatia mhuri watumishi wa Mungu wetu juu ya vipaji vya nyuso zao. Nikasikia hesabu yao waliotiwa mhuri katika kila kabila la Waisraeli, watu elfu mia moja na arubaini na nne. Wa kabila la Yuda elfu kumi na mbili waliotiwa mhuri. Wa kabila la Reubeni elfu kumi na mbili. Wa kabila la Gadi elfu kumi na mbili. Wa kabila la Asheri elfu kumi na mbili. Wa kabila la Naftali elfu kumi na mbili. Wa kabila la Manase elfu kumi na mbili. Wa kabila la Simeoni elfu kumi na mbili. Wa kabila la Lawi elfu kumi na mbili. Wa kabila la Isakari elfu kumi na mbili. Wa kabila la Zabuloni elfu kumi na mbili. Wa kabila la Yusufu elfu kumi na mbili. Wa kabila la Benyamini elfu kumi na mbili waliotiwa mhuri. Baada ya hayo nikaona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele za Mwana-kondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao; wakilia kwa sauti kuu wakisema, Wokovu una Mungu wetu aketiye katika kiti cha enzi, na Mwana-kondoo. Na malaika wote walikuwa wakisimama pande zote za kile kiti cha enzi, na za hao wazee, na za wale wenye uhai wanne, nao wakaanguka kifudifudi mbele ya kile kiti cha enzi, wakamsujudu Mungu, wakisema, Amina; Baraka na utukufu na hekima na shukrani na heshima na uweza na nguvu zina Mungu wetu hata milele na milele. Amina.