Ufunuo 1:7-17
Ufunuo 1:7-17 SRUV
Tazama, yuaja na mawingu; na kila jicho litamwona, na hao waliomchoma; na makabila yote ya dunia yataomboleza kwa ajili yake. Naam. Amina. Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema Bwana Mungu, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi. Mimi Yohana, ndugu yenu na mwenye kushiriki pamoja nanyi katika mateso na ufalme na subira ya Yesu Kristo, nilikuwa katika kisiwa kiitwacho Patmo, kwa ajili ya neno la Mungu, na ushuhuda wa Yesu. Nilikuwa katika Roho, siku ya Bwana; nikasikia sauti kuu nyuma yangu, kama sauti ya baragumu, ikisema, Haya uyaonayo uyaandike katika kitabu, ukayapeleke kwa hayo makanisa saba: Efeso, na Smirna, na Pergamo, na Thiatira, na Sardi, na Filadelfia, na Laodikia. Nikageuka niione ile sauti iliyosema nami. Na nilipogeuka, niliona vinara vya taa saba vya dhahabu; na katikati ya vile vinara nikaona mtu mfano wa Mwanadamu, amevaa vazi lililofika miguuni, na kufungwa mshipi wa dhahabu kifuani Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu nyeupe, kama theluji; na macho yake kama muali wa moto; na miguu yake kama shaba iliyosuguliwa sana, kana kwamba imesafishwa katika tanuri; na sauti yake kama sauti ya maji mengi. Naye alikuwa na nyota saba katika mkono wake wa kulia; na upanga mkali, wenye makali kuwili, ukitoka katika kinywa chake; na uso wake kama jua liking'aa kwa nguvu zake. Nami nilipomwona, nilianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kulia juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho