Zaburi 60:1-12
Zaburi 60:1-12 SRUV
Ee Mungu, umetutupa na kututawanya, Umekuwa na hasira, uturudishe tena. Umeitetemesha nchi na kuipasua, Upaponye palipobomoka, maana inatikisika. Umewaonesha watu wako mazito, Na kutunywesha mvinyo ya kutuyumbisha. Umewapa wakuogopao bendera, Ili itwekwe kwa ajili ya kweli. Ili wapenzi wako waopolewe, Utuokoe kwa mkono wako wa kulia, utuitikie. Mungu amenena kwa utakatifu wake, Nami nikishangilia. Nitaigawanya Shekemu, Na kulipima bonde la Sukothi. Gileadi ni yangu, na Manase ni yangu, Na Efraimu ni kinga ya kichwa changu. Yuda ni fimbo yangu ya kifalme, Moabu ni bakuli langu la kunawia. Nitamtupia Edomu kiatu changu, Na kumpigia Filisti kelele za vita. Ni nani atakayenipeleka hadi mji wenye boma? Ni nani atakayeniongoza hadi Edomu? Ee Mungu, si Wewe uliyetutupa? Wala, Ee Mungu, hutoki na majeshi yetu? Utuletee msaada juu ya mtesi, Maana wokovu wa binadamu haufai kitu. Kwa msaada wa Mungu tutatenda makuu, Maana Yeye atawakanyaga watesi wetu.