Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 55

55
Kusalitiwa na rafiki
Kwa mwimbishaji: kwa ala za nyuzi za muziki. Utenzi wa Daudi.
1Ee Mungu, uisikilize sala yangu,
Wala usijifiche nikuombapo rehema.
2Unisikilize na kunijibu,
Nimetangatanga nikilalama na kuugua.
3Kwa sababu ya sauti ya adui,
Kwa sababu ya dhuluma yake yule mwovu.
Kwa maana wananitupia uovu,
Na kwa ghadhabu wananiudhi.
4 # Zab 102:3-5; Mt 26:37,38; Yn 12:27; 2 Kor 1:8-10 Moyo wangu unaumia ndani yangu,
Na hofu za mauti zimeniangukia.
5Hofu na tetemeko limenijia,
Na hofu kubwa imeniingia.
6Nikasema, Ningekuwa na mbawa kama njiwa,
Ningeruka mbali na kustarehe.
7Ningekwenda zangu mbali,
Ningetua jangwani.
8Ningefanya haraka kuzikimbia
Dhoruba na tufani.
9Ee Bwana, uwaangamize, uzivuruge ndimi zao,
Maana nimeona dhuluma na fitina katika mji.
10Mchana na usiku huzunguka kutani mwake;
Uovu na taabu zimo ndani yake;
11Tamaa mbaya zimo ndani yake;
Dhuluma na hila haziondoki mitaani mwake.
12Kwa maana si adui aliyenitukana;
Kama ndivyo, ningevumilia.
Aliyejitukuza juu yangu siye anichukiaye;
Kama ndivyo, ningejificha asinione.
13 # 2 Sam 15:12 Bali ni wewe, mtu mwenzangu,
Rafiki yangu, niliyejuana nawe sana.
14Tumehusiana vizuri; na kutembea
Nyumbani mwa Mungu pamoja na mkutano.
15 # Hes 16:30 Mauti na iwapate kwa ghafla,
Na washuke kuzimu wangali hai,
Maana uovu uko nyumbani mwao moyoni mwao.
16Nami nitamwita Mungu,
Na BWANA ataniokoa;
17 # Dan 6:10; Lk 18:1; Mdo 3:1 Jioni, asubuhi, na adhuhuri nitalalama na kuugua,
Naye ataisikia sauti yangu.
18 # 2 Nya 32:7 Ameiokoa nafsi yangu iwe salama, asinikaribie mtu,
Maana walioshindana nami walikuwa wengi.
19 # Kum 33:27 Mungu atawalaye tangu milele atanisikia;
Na kuwaadhibu,
maana hawajirekebishi,
Wala kumcha Mungu.
20Mwenzangu amenyosha mkono awadhuru waliopatana naye,
Amelivunja agano lake.
21Kinywa chake ni laini kuliko siagi,
Bali moyo wake ni vita.
Maneno yake ni mororo kuliko mafuta,
Lakini yanakata kama upanga mkali.
22 # Zab 37:24 Umtwike BWANA mzigo wako naye atakutegemeza,
Hatamwacha mwenye haki aondoshwe milele.
23Nawe, Ee Mungu, utawateremsha,
Wafikie shimo la uharibifu;
Watu wa damu na hila hawataishi nusu ya siku zao,
Bali mimi nitakutumaini Wewe.

Iliyochaguliwa sasa

Zaburi 55: SRUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia