Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 139:1-18

Zaburi 139:1-18 SRUV

Ee BWANA, umenichunguza na kunijua. Wewe wajua kuketi kwangu na kusimama kwangu; Umelifahamu wazo langu tokea mbali. Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu, Umeelewa na njia zangu zote. Maana hamna neno katika ulimini wangu Usilolijua kabisa, BWANA. Umenizingira nyuma na mbele, Ukaniwekea mkono wako. Maarifa hayo ni ya ajabu, yanishinda mimi, Hayadirikiki, siwezi kuyafikia. Niende wapi nijiepushe na roho yako? Niende wapi niukimbie uso wako? Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko; Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko. Ningezitwaa mbawa za asubuhi, Na kukaa pande za mwisho za bahari; Huko nako mkono wako utaniongoza, Na mkono wako wa kulia utanishika. Kama nikisema, Hakika giza litanifunika, Na nuru inizungukayo ingekuwa usiku; Giza nalo halikufichi kitu, Bali usiku huangaza kama mchana; Giza na mwanga kwako ni sawasawa. Maana Wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu, Uliniunga tumboni mwa mama yangu. Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa Kwa njia ya ajabu ya kutisha. Matendo yako ni ya ajabu, Na nafsi yangu yajua sana, Mifupa yangu haikusitirika kwako, Nilipoumbwa kwa siri, Nilipoungwa kwa ustadi katika pande za chini za nchi; Macho yako yaliniona kabla sijakamilika; Kitabuni mwako ziliandikwa zote pia, Siku zilizoamriwa kabla hazijawa bado. Mawazo yako ni mazito sana kwangu; Ee Mungu; nayo ni makuu sana. Kama ningeyahesabu ni mengi kuliko mchanga; Niamkapo ningali pamoja nawe.

Soma Zaburi 139

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Zaburi 139:1-18