Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 119:1-96

Zaburi 119:1-96 SRUV

Heri walio kamili njia zao, Waendao katika sheria ya BWANA. Heri wazitiio shuhuda zake, Wamtafutao kwa moyo wote. Naam, hawakutenda ubatili, Wamekwenda katika njia zake. Wewe umetuamuru mausia yako, Ili sisi tuyatii sana. Ningependa njia zangu ziwe thabiti, Nizitii amri zako. Ndipo mimi sitaaibika, Nikiyaangalia maagizo yako yote. Nitakushukuru kwa unyofu wa moyo, Nikiisha kujifunza hukumu za haki yako. Nitazitii amri zako, Usiniache kabisa. Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata neno lako. Kwa moyo wangu wote nimekutafuta, Usiniache nipotee mbali na maagizo yako. Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi. Ee BWANA, umehimidiwa, Unifundishe amri zako. Kwa midomo yangu nimezisimulia Hukumu zote za kinywa chako. Nimeifurahia njia ya shuhuda zako Kana kwamba ni mali mengi. Nitayatafakari maagizo yako, Na kuziangalia njia zako. Nitajifurahisha sana kwa amri zako, Sitalisahau neno lako. Umtendee mtumishi wako ukarimu, Nipate kuishi, nami nitalitii neno lako. Unifumbue macho yangu niyatazame Maajabu yatokayo katika sheria yako. Mimi ni mgeni katika nchi, Usinifiche maagizo yako. Roho yangu imepondeka kwa kutamani Hukumu zako kila wakati. Umewakemea wenye kiburi, Wamelaaniwa waendao mbali na maagizo yako. Uniondolee laumu na dharau, Kwa maana nimezishika shuhuda zako. Wakuu nao waliketi wakaninena, Lakini mtumishi wako atazitafakari amri zako. Shuhuda zako nazo ndizo furaha yangu, Na washauri wangu. Nafsi yangu imegandamia mavumbini, Unihuishe sawasawa na neno lako. Nilizisimulia njia zangu ukanijibu, Unifundishe amri zako. Unifahamishe njia ya maagizo yako, Nami nitayatafakari maajabu yako. Nafsi yangu imeyeyuka kwa huzuni, Unitie nguvu sawasawa na neno lako. Uniondolee njia ya uongo, Unineemeshe kwa sheria yako. Nimeichagua njia ya uaminifu, Na kuziweka hukumu zako mbele yangu. Nimeambatana na shuhuda zako, Ee BWANA, usiniaibishe. Nitakwenda mbio katika njia ya maagizo yako, Utakaponipanulia ufahamu wangu. Ee BWANA, unifundishe njia ya amri zako, Nami nitaishika hadi mwisho. Unifahamishe nami nitaishika sheria yako, Naam, nitaitii kwa moyo wangu wote. Uniendeshe katika mapito ya amri zako, Kwa maana nimependezwa nayo. Unielekeze moyo wangu katika shuhuda zako, Wala usiielekee tamaa. Unigeuze macho yangu nisitazame visivyofaa, Unihuishe katika njia yako. Umthibitishie mtumishi wako ahadi yako, Iliyo ya wanaokucha. Uniondolee laumu niiogopayo, Maana hukumu zako ni njema. Tazama, nimeyatamani mausia yako, Unihuishe kwa haki yako. Ee BWANA, fadhili zako zinifikie na mimi, Naam, wokovu wako kulingana na ahadi yako. Nami nitamjibu neno anilaumuye, Kwa maana nilitumainia neno lako. Usiliondoe neno la kweli kinywani mwangu kamwe, Maana nimezingojea hukumu zako. Nami nitaitii sheria yako daima, Naam, milele na milele. Nami nitakwenda kwa uhuru, Kwa kuwa nimejifunza mausia yako. Nitazinena shuhuda zako mbele ya wafalme, Wala sitaona aibu. Nami nitajifurahisha sana kwa maagizo yako, Ambayo nimeyapenda. Na mikono yangu nitayainulia maagizo yako niliyoyapenda, Nami nitazitafakari amri zako. Likumbuke neno ulilomwambia mtumishi wako, Ambalo kwalo umenipa tumaini. Hii ndiyo faraja yangu katika taabu yangu, Ya kwamba ahadi yako imenipa moyo. Wenye kiburi wamenidharau mno, Lakini sikiuki sheria zako. Ninapozikumbuka hukumu zako za tangu kale, Ee BWANA, ninafarijika. Ghadhabu kuu imenishika kwa sababu ya wasio haki, Waiachao sheria yako. Amri zako zimekuwa nyimbo zangu, Katika nyumba yangu ya ugenini. Wakati wa usiku nimelikumbuka jina lako, Ee BWANA, nikaitii sheria yako. Hayo ndiyo niliyokuwa nayo, Kwa sababu nimeyashika mausia yako. BWANA ndiye aliye fungu langu, Ninaahidi kuyatii maneno yake. Nimekuomba radhi kwa moyo wangu wote, Unifadhili kulingana na ahadi yako. Ninapozitafakari njia zako, Naielekeza miguu yangu kwa shuhuda zako. Nilifanya haraka wala sikukawia, Kuyatii maagizo yako. Japo kamba za wasio haki zimenifunga, Siisahau sheria yako. Usiku wa manane nitaamka nikushukuru, Kwa sababu ya hukumu zako za haki. Mimi ni mwenzi wa watu wote wakuchao, Na wale wayatiio mausia yako. BWANA, dunia imejaa fadhili zako, Unifundishe amri zako. Umemtendea mtumishi wako mema, Ee BWANA, sawasawa na neno lako. Unifundishe akili na maarifa, Maana nimeyaamini maagizo yako. Kabla sijateswa mimi nilipotea, Lakini sasa nimelitii neno lako. Wewe U mwema na mtenda mema, Unifundishe amri zako. Wenye kiburi wamenizulia uongo, Lakini kwa moyo wangu wote nitayashika mausia yako. Mioyo yao imenenepa kama shahamu, Lakini mimi nimeifurahia sheria yako. Ilikuwa vema kwangu kuwa niliteswa, Nipate kujifunza amri zako. Sheria ya kinywa chako ni njema kwangu, Kuliko maelfu ya dhahabu na fedha. Mikono yako iliniumba na kunidhibiti, Unifahamishe nikajifunze amri zako. Wakuchao na wanione na kufurahi, Kwa sababu nimelitumainia neno lako. Najua ya kuwa hukumu zako ni za haki, Ee BWANA, na kwa uaminifu umenitesa. Nakuomba, fadhili zako ziwe faraja kwangu, Kulingana na ahadi yako kwa mtumishi wako. Rehema zako zinijie nipate kuishi, Maana sheria yako ni furaha yangu. Wenye kiburi waaibike, maana wamenidhulumu kwa uongo, Mimi nitayatafakari mausia yako. Wakuchao na wanirudie, Nao watazijua shuhuda zako. Moyo wangu na uwe mkamilifu katika amri zako, Nisije mimi nikaaibika. Nafsi yangu imefifia kwa kuutamani wokovu wako, Nimelitumainia neno lako. Macho yangu yamefifia kwa kuitazamia ahadi yako, Nikisema, Lini utakaponifariji? Maana nimekuwa kama kiriba katika moshi, Sikuzisahau amri zako. Siku za mtumishi wako ni ngapi, Lini utakapowahukumu wale wanaonifuatia? Wenye kiburi wamenichimbia mashimo, Ambao hawaifuati sheria yako. Amri zako zote ni za kudumu, Ninateswa bila sababu, nisaidie! Walikuwa karibu na kunikomesha katika nchi, Lakini sikuyaacha mausia yako. Uniponye kwa fadhili zako, Nami nitazishika shuhuda za kinywa chako. Ee BWANA, neno lako lasimama Imara mbinguni hata milele. Uaminifu wako upo kizazi baada ya kizazi, Umeiweka nchi, nayo imethibitika. Kwa hukumu zako vimesimama imara hata leo, Maana vitu vyote ni watumishi wako. Kama sheria yako isingalikuwa furaha yangu, Hapo ningalipotea katika mateso yangu. Hata milele sitayasahau maagizo yako, Maana kwa hayo umenihuisha. Mimi ni wako, uniokoe, Kwa maana nimejifunza mausia yako. Wasio haki wameniotea ili kunipoteza, Nitazitafakari shuhuda zako. Nimeona ukamilifu wote kuwa na mwisho, Bali amri yako haina kikomo.

Soma Zaburi 119

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Zaburi 119:1-96