Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Nehemia 12:27-47

Nehemia 12:27-47 SRUV

Basi, walipouweka wakfu ukuta wa Yerusalemu wakawatafuta Walawi katika mahali pao pote, ili kuwaleta Yerusalemu, ili waweze kusherehekea kuweka wakfu pamoja na furaha, na kwa shukrani, na kwa kuimba, kwa matoazi, vinanda na vinubi. Waimbaji wakakusanyika kutoka uwanda na viunga vya Yerusalemu, na kutoka vijiji vya Wanetofathi; tena kutoka Beth-gilgali, na toka mashamba ya Geba na Azmawethi; kwa maana waimbaji hao walikuwa wamejijengea vijiji katika viunga vya Yerusalemu. Makuhani na Walawi wakajitakasa, nao wakawatakasa watu, na malango, na ukuta. Ndipo nikawapandisha viongozi wa Yuda juu ya ukuta, nikawatenga makundi mawili makubwa ya hao walioandamana na kushukuru, liende upande wa kulia ukutani kuliendea lango la jaa; na baada yao wakaenda Hoshaya, na nusu ya wakuu wa Yuda, na Azaria, na Ezra, na Meshulamu, na Yuda, na Benyamini, na Shemaya, na Yeremia, na baadhi ya makuhani wenye baragumu; Zekaria, mwana wa Yonathani, mwana wa Shemaya, mwana wa Matania, mwana wa Mikaya, mwana wa Zakuri, mwana wa Asafu; na ndugu zake, Shemaya, Azareli, Milalai, Gilalai, Maai, Nethaneli, Yuda, na Hanani, wenye vinanda vya Daudi mtu wa Mungu; Ezra, mwandishi, akawatangulia; na kwa lango la chemchemi, wakienda moja kwa moja mbele yao, wakapanda madaraja ya mji wa Daudi, uinukapo ukuta, juu ya nyumba ya Daudi, mpaka lango la maji upande wa mashariki. Na kundi la pili wao wenye kushukuru wakaenda kuwalaki, na mimi nikafuata nyuma yao, pamoja na nusu ya watu, ukutani juu ya mnara wa tanuri, mpaka ule ukuta mpana; na juu ya lango la Efraimu, na kupita lango la kale, na lango la samaki, na mnara wa Hananeli, na mnara wa Hamea, mpaka lango la kondoo; nao wakasimama hapo langoni pa gereza. Ndivyo walivyosimama makundi mawili yao walioshukuru nyumbani mwa Mungu, na mimi, na nusu ya viongozi pamoja nami; na makuhani, Eliakimu, Maaseya, Miyamini, Mikaya, Elioenai, Zekaria na Hanania, wenye baragumu; na Maaseya, na Shemaya, na Eleazari, na Uzi, na Yehohanani, na Malkiya, na Elamu, na Ezeri. Waimbaji wakaimba kwa sauti kuu, akiwa Yezrahia msimamizi wao. Wakatoa dhabihu nyingi siku ile, wakafurahi; kwa kuwa Mungu amewafurahisha furaha kuu; na wanawake pia na watoto wakafurahi; hata ikasikika mbali sana furaha hiyo ya Yerusalemu. Na siku hiyo watu wakaagizwa juu ya vyumba vya hazina, kwa sadaka za kuinuliwa, na kwa malimbuko, na kwa zaka, ili kuzikusanya, kwa kadiri ya mashamba ya miji, sehemu zilizoamriwa katika torati za makuhani, na Walawi; kwa maana Yuda waliwafurahia makuhani na Walawi waliotumika. Wakauangalia ulinzi wa Mungu wao, na ulinzi wa kutakasika, na hao waimbaji na mabawabu vile vile, sawasawa na amri ya Daudi, na ya Sulemani mwanawe. Kwa kuwa siku za Daudi zamani, Asafu alikuwa mkuu wa waimbaji, na juu ya nyimbo za sifa na shukrani kwa Mungu. Na Israeli wote, siku za Zerubabeli, na siku za Nehemia, walitoa sehemu za waimbaji na mabawabu, kama ilivyohusika kila siku; nao wakawatakasia Walawi; na Walawi wakawatakasia wana wa Haruni.

Soma Nehemia 12