Marko 5:1-20
Marko 5:1-20 SRUV
Wakafika ng'ambo ya bahari mpaka nchi ya Wagerase. Na alipokwisha kushuka katika mashua, mara alikutana na mtu, ambaye ametoka makaburini, mwenye pepo mchafu; makao yake yalikuwa pale makaburini; wala hakuna mtu yeyote aliyeweza kumfunga tena, hata kwa minyororo; kwa sababu alikuwa amefungwa mara nyingi kwa pingu na minyororo, akaikata ile minyororo, na kuzivunjavunja zile pingu; wala hakuna mtu aliyekuwa na nguvu za kumshinda. Na sikuzote, usiku na mchana, alikuwako makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikatakata kwa mawe. Na alipomwona Yesu kwa mbali, alipiga mbio, akamsujudia; akapiga kelele kwa sauti kuu, akasema, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakuapisha kwa Mungu usinitese. Kwa sababu amemwambia, Ewe pepo mchafu, mtoke mtu huyu. Akamwuliza, Jina lako nani? Akamjibu, Jina langu ni Legioni, kwa kuwa tu wengi. Akamsihi sana asiwapeleke nje ya nchi ile. Na hapo milimani palikuwa na kundi kubwa la nguruwe, wakila. Pepo wote wakamsihi, wakisema, Tupeleke katika nguruwe, tupate kuwaingia wao. Akawapa ruhusa. Wale pepo wachafu wakatoka, wakaingia katika wale nguruwe; nalo kundi lote likateremka kwa kasi gengeni, wakaingia baharini, wapatao elfu mbili; wakafa baharini. Wachungaji wao wakakimbia, wakaieneza habari mjini na mashambani. Watu wakatoka walione lililotokea. Wakamwendea Yesu, wakamwona yule mwenye pepo, ameketi, amevaa nguo, ana akili zake, naye ndiye aliyekuwa na lile jeshi la pepo; wakaogopa. Na wale waliokuwa wameona waliwaeleza ni mambo gani yaliyompata yule mwenye pepo, na kuhusu nguruwe. Wakaanza kumsihi aondoke katika eneo lao. Naye alipokuwa akipanda katika mashua, yule aliyekuwa na pepo akamsihi kwamba awe pamoja naye; lakini hakumruhusu, bali alimwambia, Nenda zako nyumbani kwako, kwa watu wa kwenu, kawahubirie ni mambo gani makuu aliyokutendea Bwana, na jinsi alivyokurehemu. Akaenda zake, akaanza kuhubiri katika Dekapoli, ni mambo gani makuu Yesu aliyomtendea; watu wote wakastaajabu.