Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 11:1-10, 12-26

Marko 11:1-10 SRUV

Walipokaribia Yerusalemu karibu na Bethfage na Bethania, kukabili mlima wa Mizeituni, aliwatuma wawili katika wanafunzi wake, akawaambia, Nendeni mpaka kile kijiji kinachowakabili; na katika kuingia ndani yake, mara mtaona mwanapunda amefungwa, asiyepandwa na mtu bado; mfungueni, kamleteni. Na mtu akiwaambia, Mbona mnafanya hivi? Semeni, Bwana anamhitaji na mara atamrudisha tena hapa. Wakaenda zao, wakamwona mwanapunda amefungwa penye mlango, nje katika njia kuu, wakamfungua. Baadhi ya watu waliosimama huko wakawaambia, Mnafanya nini kumfungua mwanapunda? Wakawaambia kama Yesu alivyowaagiza, nao wakawaruhusu. Wakamletea Yesu yule mwanapunda, wakatandika mavazi yao juu yake; akaketi juu yake. Watu wengi wakatandaza mavazi yao njiani, na wengine matawi waliyoyakata mashambani. Nao watu waliotangulia na wale waliofuata wakapaza sauti, Hosana; ndiye mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana; umebarikiwa na ufalme ujao, wa baba yetu Daudi. Hosana juu mbinguni.

Soma Marko 11

Marko 11:12-26 SRUV

Siku iliyofuata walipokuwa wakitoka Bethania, aliona njaa. Akaona kwa mbali mtini wenye majani, akaenda ili labda aone kitu juu yake; na alipoufikia hakuona kitu ila majani; maana si wakati wa tini. Akajibu, akauambia, Tangu leo hata milele mtu asile matunda kwako. Wanafunzi wake wakasikia. Wakafika Yerusalemu, naye akaingia ndani ya hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakiuza na kununua ndani ya hekalu, akazipindua meza za wabadili fedha, na viti vyao wauzao njiwa; wala hakumruhusu mtu yeyote kupitia katika hekalu akiwa amebeba kitu. Akafundisha, akasema, Je! Haikuandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote? Bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi. Wakuu wa makuhani na waandishi wakapata habari wakatafuta jinsi ya kumwangamiza; maana walimwogopa, kwa sababu mkutano wote walishangazwa na mafundisho yake. Na kulipokuwa jioni alitoka mjini. Na asubuhi walipokuwa wakipita, waliuona ule mtini umenyauka toka shinani. Petro akakumbuka habari yake, akamwambia, Rabi, tazama, mtini ulioulaani umenyauka. Yesu akajibu, akamwambia, Mwaminini Mungu. Amin, nawaambia, yeyote atakayeuambia mlima huu, Ng'oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake. Kwa sababu hiyo nawaambia, Yoyote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu. Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. [ Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.]

Soma Marko 11

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Marko 11:1-10, 12-26

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha