Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mika 3:1-12

Mika 3:1-12 SRUV

Nikasema, Tafadhali sikieni, enyi vichwa vya Yakobo, mnaoitawala nyumba ya Israeli. Je! Haiwapasi ninyi kujua hukumu? Ninyi mnaoyachukia mema, na kuyapenda mabaya; ninyi mnaowachuna watu ngozi yao, na nyama mifupani mwao. Naam, mnakula nyama ya watu wangu, na kuwachuna ngozi zao, na kuivunja mifupa yao; naam, kuwakata vipande vipande kama kwa kutiwa chunguni, na kama nyama sufuriani. Ndipo watakapomwomba BWANA, asiwaitikie; naam, atawaficha uso wake wakati huo, kwa kadiri walivyotenda mabaya kwa matendo yao. BWANA asema hivi kuhusu manabii wanaowakosesha watu wangu; hao waumao kwa meno yao, na kulia, Amani; na mtu awaye yote asiyetia kitu vinywani mwao, wao humwandalia vita. Kwa hiyo itakuwa usiku kwenu, msipate kuona maono; tena itakuwa giza kwenu, msiweze kubashiri; nalo jua litawachwea manabii, nao mchana utakuwa mweusi juu yao. Na hao waonaji wataaibika, na wenye kubashiri watafadhaika; naam, hao wote watajifunika midomo yao; kwa maana; hapana jawabu la Mungu. Bali mimi, hakika nimejaa nguvu kwa Roho ya BWANA; nimejaa hukumu na uwezo; nimhubirie Yakobo kosa lake, na Israeli dhambi yake. Sikieni haya, tafadhali, enyi vichwa vya nyumba ya Yakobo, mnaoitawala nyumba ya Israeli, mnaochukia hukumu, na kuipotosha adili. Wanaoijenga Sayuni kwa damu, na Yerusalemu kwa uovu. Wakuu wake huhukumu ili wapate rushwa, na makuhani wake hufundisha ili wapate ijara, na manabii wake hubashiri ili wapate fedha; ila hata hivyo watamtegemea BWANA, na kusema, Je! Hayupo BWANA katikati yetu? Hapana neno baya lolote litakalotufikia. Basi, kwa ajili yenu, Sayuni utalimwa kama shamba lilimwavyo, na Yerusalemu utakuwa magofu; na mlima wa nyumba utakuwa kama mahali palipoinuka msituni.

Soma Mika 3

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha