Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 5:1-26

Mathayo 5:1-26 SRUV

Naye alipowaona makundi ya watu, alipanda mlimani; na alipokwisha kuketi, wanafunzi wake walimjia; akafumbua kinywa chake, akawafundisha, akisema, Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri wenye huzuni; Maana hao watafarijika. Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi. Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa. Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema. Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu. Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu. Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; Maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu. Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikipoteza ladha yake, ladha hiyo itarudishwa vipi? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu. Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji ukiwa juu ya mlima hauwezi kusitirika. Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni. Msidhani ya kuwa nilikuja kuitangua Torati au Manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yote yatimie. Basi mtu yeyote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni. Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya Waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue, na mtu akiua, itampasa hukumu. Bali mimi nawaambieni, Kila amkasirikiaye ndugu yake itampasa hukumu; na mtu akimtusi ndugu yake, anastahili kuhukumiwa na baraza; na mtu akimwambia nduguye, Ewe mpumbavu, anastahili kuingia katika moto wa Jehanamu. Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako. Patana na mshitaki wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije akakupeleka kwa hakimu, na hakimu akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani. Amin, nakuambia, Hutoki humo kamwe hadi utakapolipa senti ya mwisho.

Soma Mathayo 5