Luka 6:37-45
Luka 6:37-45 SRUV
Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; sameheni, nanyi mtasamehewa. Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa. Akawaambia mithali, Je! Aliye kipofu aweza kuongoza kipofu? Hawatatumbukia shimoni wote wawili? Mwanafunzi hawi mkuu kuliko mwalimu wake, lakini kila mtu ambaye amehitimu hulingana na mwalimu wake. Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Au, utawezaje kumwambia ndugu yako, Ndugu yangu, niache nikitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako, nawe huiangalii boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe, ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi kilichomo katika jicho la ndugu yako. Kwa maana hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala mti mbaya uzaao matunda mazuri; kwa kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake; maana, katika miiba hawachumi tini, wala katika michongoma hawachumi zabibu. Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake.