Luka 23:1-12
Luka 23:1-12 SRUV
Kisha mkutano wote wakasimama, wakampeleka kwa Pilato. Wakaanza kumshitaki, wakisema, Tumemwona huyu akipotosha taifa letu, na kuwazuia watu wasimpe Kaisari kodi, akisema kwamba yeye mwenyewe ni Kristo, mfalme. Pilato akamwuliza, akisema, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Akajibu akamwambia, Wewe wasema. Pilato akawaambia wakuu wa makuhani na mkutano, Sioni neno lililo ovu katika mtu huyu. Nao walisisitiza sana, wakisema, Huwataharakisha watu, akifundisha katika Yudea yote, tokea Galilaya mpaka huku. Pilato aliposikia hayo aliuliza kama huyu ni mtu wa Galilaya. Na alipopata habari ya kuwa yu chini ya mamlaka ya Herode, alimpeleka kwa Herode, kwa kuwa yeye naye alikuwapo Yerusalemu siku zile. Herode alipomwona Yesu alifurahi sana, kwa sababu alikuwa akitaka sana kumwona tangu siku nyingi, maana amesikia habari zake, akatarajia kuona ishara iliyofanywa na yeye. Akamwuliza maneno mengi, yeye asimjibu lolote. Wakuu wa makuhani na waandishi wakasimama wakamshitaki kwa nguvu sana. Basi Herode akamdhalilisha, pamoja na askari wake, akamdhihaki, na kumvika mavazi mazuri; kisha akamrudisha kwa Pilato. Basi siku ile ile Herode na Pilato walipatana kwa urafiki kwa maana hapo kwanza walikuwa na uadui wao kwa wao.