Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yoeli 2:1-11

Yoeli 2:1-11 SRUV

Pigeni tarumbeta katika Sayuni, Pigeni na kelele katika mlima wangu mtakatifu; Wenyeji wote wa nchi na watetemeke; Kwa maana siku ya BWANA inakuja. Kwa sababu inakaribia; siku ya giza na huzuni, siku ya mawingu na giza kuu. Kama mapambazuko yakitandazwa juu ya milima, hao ni wakuu, tena wenye nguvu, mfano wao haukuwako kamwe, wala hautakuwako baada ya hao, hata katika miaka ya vizazi vingi. Moto unaunguza vikali mbele yao; na nyuma yao miali ya moto inateketeza; hiyo nchi inafanana na bustani ya Edeni mbele yao, na nyuma yao imekuwa jangwa tupu; naam, hakuna aliyeokoka asipatikane nao. Kuonekana kwao ni kama kuonekana kwa farasi; na kama wapanda farasi ndivyo wanavyopiga mbio. Kama mshindo wa magari ya vita juu ya vilele vya milima, ndivyo warukavyo; kama mshindo wa miali ya moto iunguzapo mabua makavu, kama mashujaa waliopangwa tayari kwa vita. Mbele yao watu wanahangaika; nyuso zote zimegeuka kuwa nyeupe kwa hofu. Hupiga mbio kama mashujaa; huupanda ukuta kama watu wa vita; nao huendelea mbele kila mmoja katika njia zake, wala hawapotoshi safu zao. Wala hapana mmoja amsukumaye mwenzake; huendelea mbele kila mmoja katika njia yake; hujifanyia njia kwa nguvu kati ya silaha, wala hawaachi kuifuata njia yao. Huurukia mji; hupiga mbio juu ya ukuta; hupanda na kuingia ndani ya nyumba; huingia madirishani kama aingiavyo mwizi. Nchi inatetemeka mbele yao; mbingu zinatetemeka; jua na mwezi hutiwa giza, na nyota huacha kuangaza; naye BWANA anatoa sauti yake mbele ya jeshi lake; maana matuo yake ni makubwa sana; kwa maana yeye ni hodari atekelezaye neno lake; kwa kuwa siku ya BWANA ni kuu, yenye kitisho sana; naye ni nani awezaye kuistahimili?

Soma Yoeli 2

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Yoeli 2:1-11