Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ayubu 18:1-21

Ayubu 18:1-21 SRUV

Ndipo Bildadi, Mshuhi, akajibu, na kusema, Je! Hata lini utayawinda maneno kwa mitego? Fikiri, kisha baadaye tutanena. Twahesabiwa kuwa wanyama kwa sababu gani, Tena kuwa wanajisi machoni pako? Wewe ujiraruaye mwenyewe katika hasira yako, Je! Dunia itaachwa kwa ajili yako wewe? Au jabali litaondolewa mahali pake? Naam, mwanga wa waovu utazimika, Wala muali wa moto wake hautang'aa. Mwanga hemani mwake utakuwa giza, Nayo taa iliyo juu yake itazimwa. Hatua zake za nguvu zitasongwa, Na shauri lake mwenyewe litamwangusha chini. Kwani ametupwa katika wavu na miguu yake mwenyewe, Naye huenda juu ya matanzi. Tanzi litamshika kisigino chake, Na mtego utamshika. Amefichiwa tanzi chini, Na mtego amewekewa njiani. Vitisho vitamtia hofu kutoka kila upande, Na kumfukuza karibu na visigino vyake. Nguvu zake zitaliwa na njaa, Na msiba utakuwa tayari kwa kusita kwake. Utakula via vya mwili wake, Naam, mzaliwa wa kwanza wa mauti atavila via vyake. Atang'olewa katika hema yake aliyokuwa akiitumaini; Naye atapelekwa kwake mfalme wa vitisho. Katika hema yake hakuna kitakachobaki; Kiberiti kitamwagwa juu ya makazi yake. Chini, mizizi yake itakaushwa; Na juu, tawi lake litasinyaa. Kumbukumbu lake litakoma katika nchi, Wala hatakuwa na jina mashambani. Atakimbizwa kutoka mwangani hata gizani, Na kufukuzwa atoke duniani. Hatakuwa na mwana wala mjukuu kati ya watu wake, Wala hatasalia mtu hapo alipokaa. Hao wanaokaa magharibi watastaajabia siku yake, Kama vile wanaokaa mashariki walivyotiwa hofu. Hakika ndivyo yalivyo makazi ya wapotovu, Na hapa ni mahali pake asiyemjua Mungu.

Soma Ayubu 18