Yohana 7:1-31
Yohana 7:1-31 SRUV
Na baada ya hayo Yesu alikuwa akitembea katika Galilaya; maana hakutaka kutembea katika Yudea, kwa sababu Wayahudi walikuwa wakitaka kumwua. Na sikukuu ya Wayahudi, sikukuu ya vibanda, ilikuwa karibu. Basi ndugu zake wakamwambia, Ondoka hapa, uende Yudea, wanafunzi wako nao wapate kuzitazama kazi zako unazozifanya. Kwa maana hakuna mtu afanyaye mambo kwa siri, naye yeye mwenyewe anataka kujulikana. Ukifanya mambo haya, basi jidhihirishe kwa ulimwengu. Maana hata nduguze hawakumwamini. Basi Yesu akawaambia, Wakati wangu haujafika bado; ila wakati wenu sikuzote upo. Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi; bali hunichukia mimi, kwa sababu mimi naushuhudia ya kuwa kazi zake ni mbovu. Pandeni ninyi kwenda kula sikukuu; mimi sipandi bado kwenda kula sikukuu hii, kwa kuwa wakati wangu haujatimia. Naye alipokwisha kuwaambia hayo, alibaki huko Galilaya. Hata ndugu zake walipokwisha kupanda kuiendea sikukuu, ndipo yeye naye alipopanda, si kwa wazi bali kana kwamba kwa siri. Basi Wayahudi wakamtafuta kwenye sikukuu, wakasema, Yuko wapi yule? Kukawa na manung'uniko mengi katika makutano juu yake. Wengine wakasema, Ni mtu mwema. Na wengine wakasema, Sivyo; bali anawadanganya makutano. Lakini hakuna mtu aliyemsema waziwazi, kwa sababu ya kuwaogopa Wayahudi. Hata ikawa katikati ya sikukuu Yesu alipanda kuingia hekaluni, akafundisha. Wayahudi wakastaajabu wakisema, Amepataje huyu kujua elimu, ambaye hakusoma? Basi Yesu akawajibu, akasema, Mafunzo yangu si yangu mimi, ila ni yake yeye aliyenituma. Mtu akipenda kuyatenda mapenzi yake, atajua habari ya yale mafunzo, kwamba yatoka kwa Mungu, au kwamba mimi nanena kwa nafsi yangu tu. Yeye anenaye kwa nafsi yake tu hutafuta utukufu wake mwenyewe; bali yeye anayetafuta utukufu wake aliyemtuma, huyo ni wa kweli, wala ndani yake hamna udhalimu. Je! Musa hakuwapa torati? Wala hakuna mmoja wenu aitendaye torati. Mbona mnatafuta kuniua? Mkutano wakajibu, Ama! Una pepo! Ni nani anayetafuta kukuua? Yesu akajibu, akawaambia, Mimi nilitenda kazi moja, nanyi nyote mnaistaajabia. Musa aliwapa tohara; lakini si kwamba yatoka kwa Musa, bali kwa mababa; nanyi mwatahiri mtu siku ya sabato. Basi ikiwa mtu hupashwa tohara siku ya sabato, ili Torati ya Musa isije ikavunjika, mbona mnanikasirikia mimi kwa sababu nilimfanya mtu kuwa mzima kabisa siku ya sabato? Basi msihukumu kwa kuangalia kwa nje tu, bali ifanyeni hukumu iliyo ya haki. Basi baadhi ya watu wa Yerusalemu wakasema, Je! Huyu siye wanayemtafuta ili wamwue? Na kumbe! Anena waziwazi, wala hawamwambii neno! Inawezekana hao wakuu wanajua hakika ya kuwa huyu ndiye Kristo? Lakini huyu twamjua atokako; bali Kristo atakapokuja hakuna ajuaye atokako. Basi Yesu akapaza sauti yake hekaluni, akifundisha na kusema, Mimi mnanijua, na huko nitokako mnakujua; wala sikuja kwa nafsi yangu; ila yeye aliyenituma ni wa kweli, msiyemjua ninyi. Mimi namjua, kwa kuwa nimetoka kwake, naye ndiye aliyenituma. Basi wakatafuta kumkamata; lakini hakuna mtu aliyeunyosha mkono wake ili kumshika, kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado. Na watu wengi katika mkutano wakamwamini; wakasema, Atakapokuja Kristo, je! Atafanya ishara nyingi zaidi kuliko hizi alizozifanya huyu?