Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 19:1-27

Yohana 19:1-27 SRUV

Basi ndipo Pilato alipomtwaa Yesu, akampiga mijeledi. Nao askari wakasokota taji la miiba, wakamtia kichwani, wakamvika vazi la zambarau. Wakawa wakimwendea, wakisema, Salamu! Mfalme wa Wayahudi! Wakampiga makofi. Kisha Pilato akatokea tena nje, akawaambia, Mtu huyu namleta nje kwenu, mpate kufahamu ya kuwa mimi sioni hatia yoyote kwake. Ndipo Yesu alipotoka nje, naye amevaa lile taji la miiba, na lile vazi la zambarau. Pilato akawaambia, Tazama, mtu huyu! Basi wale wakuu wa makuhani na watumishi wao walipomwona, walipiga kelele wakisema, Msulubishe! Msulubishe! Pilato akawaambia, Mtwaeni ninyi basi, mkamsulubishe; kwa maana mimi sioni hatia kwake. Wayahudi wakamjibu, Sisi tunayo sheria, na kwa sheria hiyo amestahili kufa, kwa sababu alijifanya kuwa Mwana wa Mungu. Basi Pilato aliposikia neno hilo, akazidi kuogopa. Akaingia tena ndani ya ile Praitorio, akamwambia Yesu, Wewe umetoka wapi? Lakini Yesu hakumpa jibu lolote. Basi Pilato akamwambia, Husemi nami? Hujui ya kuwa mimi nina mamlaka ya kukufungua, nami nina mamlaka ya kukusulubisha? Yesu akamjibu, Wewe hungekuwa na mamlaka yoyote juu yangu, kama usingepewa kutoka juu; kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi mwako ana dhambi iliyo kubwa zaidi. Na tangu hapo Pilato akatafuta kumfungua; lakini Wayahudi wakapiga makelele wakisema, Ukimfungua huyu, wewe si rafiki yake Kaisari; kila mtu ajifanyaye kuwa mfalme humfitini Kaisari. Basi Pilato, aliposikia maneno hayo, akamleta Yesu nje, akaketi juu ya kiti cha hukumu, mahali paitwapo Sakafu ya Mawe, au kwa Kiebrania, Gabatha. Nayo ilikuwa Maandalio ya Pasaka, yapata saa sita. Akawaambia Wayahudi, Tazama, Mfalme wenu! Basi wale wakapiga kelele, Mwondoshe! Mwondoshe! Msulubishe! Pilato akawaambia, Je! Nimsulubishe mfalme wenu! Wakuu wa makuhani wakamjibu, Sisi hatuna mfalme ila Kaisari. Basi ndipo alipomtia mikononi mwao ili asulubiwe; nao wakampokea Yesu. Akatoka, huku akijichukulia msalaba wake, mpaka mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, au kwa Kiebrania, Golgotha. Wakamsulubisha huko, na wengine wawili pamoja naye, mmoja huku na mmoja huku, na Yesu katikati. Naye Pilato akaandika anwani, akaiweka juu ya msalaba, imeandikwa, YESU MNAZARETI, MFALME WA WAYAHUDI. Basi anwani hiyo waliisoma wengi katika Wayahudi; maana mahali pale aliposulubiwa Yesu palikuwa karibu na mji; nayo iliandikwa kwa Kiebrania, na Kirumi, na Kigiriki. Basi wakuu wa makuhani na Wayahudi wakamwambia Pilato, Usiandike, Mfalme wa Wayahudi; bali ya kwamba yule alisema, Mimi ni mfalme wa Wayahudi. Pilato akajibu, Niliyoandika nimeyaandika. Nao askari walipomsulubisha Yesu, waliyatwaa mavazi yake, wakafanya mafungu manne, kwa kila askari fungu lake; na kanzu nayo. Basi kanzu ile haikushonwa, ilikuwa imefumwa yote pia tangu juu. Basi wakaambiana, Tusiipasue, lakini tuipigie kura, iwe ya nani. Ili litimie andiko lile linenalo, Waligawanya nguo zangu, Na vazi langu wakalipigia kura. Basi ndivyo walivyofanya wale askari. Na penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mamaye, na umbu la mamaye, Mariamu wa Klopa, na Mariamu Magdalene. Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao. Kisha akamwambia yule mwanafunzi, Tazama, mama yako. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake.

Soma Yohana 19

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Yohana 19:1-27

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha