Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 10:1-18

Yohana 10:1-18 SRUV

Yesu aliwaambia, Amin, amin, nawaambieni, Yeye asiyeingia mlangoni katika zizi la kondoo, lakini akwea penginepo, huyo ni mwizi naye ni mnyang'anyi. Aingiaye mlangoni ni mchungaji wa kondoo. Bawabu humfungulia huyo, na kondoo humsikia sauti yake; naye huwaita kondoo wake kwa majina yao, na kuwapeleka nje. Naye awatoapo nje kondoo wake wote, huwatangulia; na wale kondoo humfuata, kwa maana waijua sauti yake. Mgeni hawatamfuata kabisa, bali watamkimbia; kwa maana hawazijui sauti za wageni. Mithali hiyo Yesu aliwaambia, lakini wao hawakuelewa mambo hayo aliyowaambia. Basi Yesu aliwaambia tena, Amin, amin, nawaambieni, Mimi ndimi mlango wa kondoo. Wote walionitangulia ni wezi na wanyang'anyi; lakini kondoo hawakuwasikia. Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho. Mwizi huja tu kuiba, kuua na kuharibu; mimi nilikuja ili wawe na uzima, tena wawe nao tele. Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Mtu wa mshahara, wala si mchungaji, ambaye kondoo si mali yake, humwona mbwamwitu anakuja, akawaacha kondoo na kukimbia; na mbwamwitu huwakamata na kuwatawanya. Yule hukimbia kwa kuwa ni mtu wa mshahara; wala mambo ya kondoo si kitu kwake. Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi; kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo. Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja. Ndiposa Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena. Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi nautoa mwenyewe. Nami ninao uweza wa kuutoa, ninao na uweza wa kuutwaa tena. Agizo hilo nililipokea kwa Baba yangu.

Soma Yohana 10

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Yohana 10:1-18

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha