Hosea 2:14-23
Hosea 2:14-23 SRUV
Kwa hiyo angalia, mimi nitamshawishi, na kumleta nyikani, na kusema naye maneno ya kumtuliza moyo. Nami nitampa mashamba yake ya mizabibu toka huko, na bonde la Akori kuwa mlango wa tumaini; naye ataniitikia huko, kama siku zile za ujana wake, na kama siku ile alipopanda kutoka nchi ya Misri. Tena siku hiyo itakuwa, asema BWANA, utaniita Ishi, wala hutaniita tena Baali. Kwa maana nitayaondoa majina ya Mabaali kinywani mwake, wala hawatatajwa tena kwa majina yao. Nami siku hiyo nitafanya agano na wanyama wa mashamba kwa ajili yao, tena na ndege wa angani, tena na wadudu wa nchi; nami nitavivunja upinde na upanga na silaha vitoke katika nchi, nami nitawalalisha salama salimini. Nami nitakuposa uwe wangu wa milele; naam, nitakuposa kwa haki, na kwa hukumu, na kwa ufadhili, na kwa rehema. Nami nitakuposa kwa uaminifu; nawe utamjua BWANA. Tena itakuwa siku hiyo, mimi nitaitika, asema BWANA; nitaziitikia mbingu, nazo zitaiitikia nchi; nayo nchi itaiitikia nafaka na divai na mafuta; nayo yataiitikia Yezreeli. Nami nitampanda katika nchi kwa ajili yangu mwenyewe; nami nitamrehemu yeye asiyepewa rehema; nami nitawaambia wale wasiokuwa watu wangu, Ninyi ndinyi watu wangu; nao watasema, Wewe ndiwe Mungu wangu.