Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waraka kwa Waebrania 6:1-12

Waraka kwa Waebrania 6:1-12 SRUV

Kwa sababu hiyo, tukiacha kuyanena mafundisho ya kwanza ya Kristo, tukaze mwendo ili tuufikie utimilifu; tusiweke msingi tena wa kuzitubia kazi zisizo na uhai, na wa kuwa na imani kwa Mungu, na wa mafundisho ya ubatizo, na kuwekea mikono, na kufufuliwa wafu, na hukumu ya milele. Na hayo tutafanya Mungu akitujalia. Kwa maana hao waliokwisha kupewa nuru, na kukionja kipawa cha mbinguni, na kufanywa washirika wa Roho Mtakatifu, na kulionja neno zuri la Mungu, na nguvu za wakati ujao, wakaanguka baada ya hayo, haiwezekani kuwafanya upya tena hata wakatubu; kwa kuwa wamsulubisha Mwana wa Mungu mara ya pili kwa nafsi zao, na kumtweza hadharani kwa dhahiri. Maana nchi inayoinywa mvua inayoinyeshea mara kwa mara, na kuzaa mboga zenye manufaa kwa hao ambao kwa ajili yao inalimwa, hupokea baraka zitokazo kwa Mungu; bali ikitoa miiba na magugu hukataliwa na kuwa karibu na laana; ambayo mwisho wake ni kuteketezwa. Lakini, wapenzi, ijapokuwa twanena hayo, kuhusu habari zenu tumeamini mambo yaliyo mazuri zaidi, na yaliyo na wokovu. Maana Mungu si dhalimu hata aisahau kazi yenu, na pendo lile mlilolidhihirisha kwa jina lake, kwa kuwa mmewahudumia watakatifu, na hata hivi sasa mngali mkiwahudumia. Nasi twataka sana kila mmoja wenu aidhihirishe bidii ile ile, kwa utimilifu wa matumaini hata mwisho; ili msiwe wavivu, bali mkawe kama hao wazirithio ahadi kwa imani na uvumilivu.