Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 50:1-26

Mwanzo 50:1-26 SRUV

Yusufu akamwangukia babaye usoni, akamlilila, akambusu. Yusufu akawaagiza watumishi wake waganga wampake baba yake dawa asioze. Waganga wakampaka dawa Israeli. Siku zake arubaini zikaisha, maana siku hizo zilitimiza siku za wale waliohifadhiwa kwa kupakwa dawa. Wamisri wakamwombolezea siku sabini. Siku za kumwombolezea zilipopita, Yusufu alisema na watu wa nyumba ya Farao, akinena, Kama nimeona neema machoni penu, tafadhalini mkaseme masikioni mwa Farao, mkinena, Baba yangu aliniapisha, akisema, Mimi ni katika kufa, unizike katika kaburi langu nililojichimbia katika nchi ya Kanaani. Basi tafadhali uniruhusu niende sasa nikamzike babangu, nami nitarudi. Farao akasema, Nenda, ukamzike baba yako, kama alivyokuapisha. Basi Yusufu akaenda kumzika baba yake, na watumishi wote wa Farao wakaenda pamoja naye, wazee wa nyumbani mwake, na wazee wote wa nchi ya Misri. Na nyumba yote ya Yusufu, na ndugu zake, na nyumba ya baba yake; wakawaacha watoto wao tu, na kondoo wao, na ng'ombe wao, katika nchi ya Gosheni. Kisha wakaenda pamoja naye wapanda farasi, na magari; wakawa jeshi kubwa sana. Wakaja mpaka uwanja wa kupuria nafaka wa Atadi, uliyo ng'ambo ya Yordani. Wakaomboleza huko maombolezo makuu, mazito sana. Akafanya matanga ya baba yake siku saba. Nao waliokaa katika nchi, wale Wakanaani, walipoyaona matanga katika sakafu ya Atadi, wakasema, Matanga haya ya Wamisri ni makuu kwa hiyo mahali pale paliitwa Abel-Misri, iliyo ng'ambo ya Yordani. Wanawe wakamfanyia kama alivyowaagiza; kwa kuwa wanawe wakamchukua mpaka nchi ya Kanaani, na wakamzika katika pango ya shamba la Makpela, iliyo mbele ya Mamre, aliyoinunua Abrahamu pamoja na shamba kwa Efroni Mhiti, pawe milki yake ya kuzikia. Yusufu akarudi Misri, yeye na ndugu zake, na wote waliokwenda pamoja naye kumzika baba yake, baada ya kumzika baba yake. Ndugu zake Yusufu walipoona ya kwamba baba yao amekufa, walisema, Labda Yusufu atatuchukia; naye atatulipa maovu yetu tuliyomtenda. Wakatuma watu kwa Yusufu, kunena, Baba yako alitoa amri kabla ya kufa kwake, akasema, Mwambieni Yusufu hivi, Naomba uwasamehe ndugu zako kosa lao na dhambi yao, maana walikutenda mabaya; sasa twakuomba utusamehe kosa la watumishi wa Mungu wa baba yako. Yusufu akalia waliposema naye. Ndugu zake wakaenda tena, wakamwangukia miguu, wakasema, Tazama, sisi tu watumishi wako. Yusufu akawaambia, Msiogope, je! Mimi ni badala ya Mungu? Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo. Basi sasa msiogope; mimi nitawalisha na watoto wenu. Akawafariji, na kusema nao vema. Yusufu Akakaa katika Misri, yeye na nyumba ya baba yake. Yusufu Akaishi miaka mia moja na kumi. Yusufu akaona wana wa Efraimu hata kizazi cha tatu; na wana wa Makiri, mwana wa Manase, walizaliwa magotini mwa Yusufu. Yusufu akawaambia ndugu zake, Mimi ninakufa, lakini Mungu atawajia ninyi bila shaka, atawapandisha toka nchi hii, mpaka nchi aliyowaapia Abrahamu, na Isaka, na Yakobo. Yusufu akawaapisha wana wa Israeli, akasema, Bila shaka Mungu atawajia ninyi, nanyi mtaipandisha huko mifupa yangu. Basi Yusufu akafa, mwenye miaka mia moja na kumi; wakampaka dawa, wakamtia katika sanduku, huko Misri.

Soma Mwanzo 50

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha