Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 37

37
Ndoto za Yusufu
1 # Mwa 36:7 Yakobo akakaa katika nchi aliyosafiri baba yake, katika nchi ya Kanaani. 2#1 Sam 2:22-24 Hivi ndivyo vizazi vya Yakobo. Yusufu, aliyekuwa mwenye miaka kumi na saba, alikuwa akichunga kondoo pamoja na ndugu zake; naye alikuwa kijana pamoja na wana wa Bilha, na wana wa Zilpa, wake wa baba yake. Yusufu akamletea baba yao habari zao mbaya. 3#2 Sam 13:18 Basi Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. 4#Mwa 27:41; 49:23; 1 Sam 17:28; Yn 7:3,5; 1 Yoh 2:11; 3:10 Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani.
5Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia; 6akawaambia, Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota. 7#Mwa 42:6; 43:26; 44:14 Tazama, sisi tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka ukasimama, na tazama, miganda yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu. 8Ndugu zake wakamwambia, Je! Kweli wewe utatumiliki sisi? Nawe utatutawala sisi? Wakazidi kumchukia kwa ajili ya ndoto yake, na kwa maneno yake.
9 # Mwa 46:29 Akaota tena ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake, akasema, Angalieni, nimeota ndoto nyingine; na tazama, jua na mwezi na nyota kumi na moja zikaniinamia. 10#Mwa 27:29 Akawaambia baba yake na ndugu zake; baba yake akamkemea akamwambia, Ni ndoto gani hii uliyoiota? Je! Mimi na mama yako na ndugu zako tutakuja tukusujudie mpaka chini? 11#Mdo 7:9; Lk 2:19,51 Ndugu zake wakamhusudu; bali baba yake akalihifadhi neno hili.
Yusufu auzwa na ndugu zake
12Ndugu zake wakaenda kuchunga kondoo za baba yao huko Shekemu. 13Israeli akamwambia Yusufu, Je! Ndugu zako hawachungi kondoo katika Shekemu? Njoo, nikutume kwao. Akamwambia, Mimi hapa. 14#Mwa 29:6; 1 Sam 17:18; Mwa 13:18 Akamwambia, Nenda, basi, ukaone kama ndugu zako hawajambo, na kundi nalo li salama, ukaniletee habari. Basi akamtuma kutoka bonde la Hebroni, na akafika Shekemu.
15Mtu mmoja akamkuta, naye alikuwa anazungukazunguka katika nyika; yule mtu akamwuliza, akisema, Unatafuta nini? 16#Wim 1:7 Akasema, Nawatafuta ndugu zangu; tafadhali uniambie mahali wanakochunga. 17#2 Fal 6:13 Yule mtu akasema, Wametoka hapa, maana niliwasikia wakisema, Twendeni Dothani. Basi Yusufu akawafuata ndugu zake akawakuta huko Dothani. 18#1 Sam 19:1; Zab 31:13; Mt 27:1; Mk 14:1; Yn 11:53; Mdo 23:12 Wakamwona akiwa mbali, na kabla hajawakaribia, wakafanya shauri juu yake ili wamwue. 19Wakasemezana wao kwa wao, Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja. 20#Mit 1:11; 6:17; 1 Yoh 3:12,13 Haya, twende, tukamwue na kumtupa katika shimo mojawapo, nasi tutasema, Mnyama mkali amemla; kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake.
21 # Mwa 42:22 Reubeni akasikia akamwokoa katika mikono yao, akasema, Tusimwue. 22Reubeni akawaambia, Msimwage damu; mtupeni katika shimo hili lililopo nyikani, wala msimguse; ili apate kumwokoa katika mikono yao, akamrudishe kwa baba yake. 23Ikawa Yusufu alipofika kwa ndugu zake, wakamvua Yusufu kanzu yake, kanzu ile ndefu aliyoivaa, 24wakamtwaa wakamtupa katika shimo; na hilo shimo ilikuwa tupu, hamna maji. 25#Mit 30:20; Amo 6:6; Yer 8:22 Nao wakakaa kitako kula chakula; wakainua macho yao, wakaona, msafara wa Waishmaeli wanakuja wakitoka Gileadi na ngamia zao, wakichukua ubani na zeri na manemane, wakisafiri kuvichukua mpaka Misri. 26#Mwa 4:10; Ayu 16:18 Yuda akawaambia ndugu zake, Kwafaa nini kumwua ndugu yetu, na kuificha damu yake? 27#1 Sam 18:17; Mwa 29:14; 42:21 Haya, na tumuuze kwa hawa Waishmaeli, wala mikono yetu isimdhuru, maana yeye ni ndugu yetu, na damu yetu. Ndugu zake wakakubali. 28#Mdo 7:9; Mwa 39:1; Amu 6:3; Mwa 45:4,5; Zab 105:17; Mt 27:9 Wakapita wafanya biashara Wamidiani; basi wakamtoa Yusufu, wakampandisha kumtoa katika shimo, wakamuuza Yusufu kwa Waishmaeli kwa vipande vya fedha ishirini; nao wakamchukua Yusufu mpaka Misri.
29 # Ayu 1:20 Akarudi Reubeni birikani, kumbe! Yusufu hayumo katika birika, akararua nguo zake. 30#Yer 31:15; Mwa 42:13,36 Akarudi kwa ndugu zake, akasema, Mtoto hayuko, nami niende wapi? 31Wakaitwaa kanzu ya Yusufu, wakachinja mwana-mbuzi, na kuichovya kanzu katika damu. 32#Mwa 37:23 Wakaenda nayo ile kanzu ndefu, wakamletea baba yao, wakasema, Tumeona hii; basi, utambue kama kanzu hii ni ya mwanao, ama siyo. 33#Mwa 44:28 Akaitambua, akasema, Ndiyo kanzu ya mwanangu, mnyama mkali amemla; bila shaka Yusufu ameraruliwa. 34#Mwa 37:29 Yakobo akararua mavazi yake, akajivika gunia viunoni, na kumlilia mwanawe siku nyingi. 35#2 Sam 12:17; Mwa 42:38 Wanawe wote, na binti zake wote, wakaondoka wamtulize, lakini akakataa kutulizwa, akasema, La! Nitashuka kaburini kwa mwanangu, nikiomboleza. Basi baba yake akamlilia. 36#Mwa 39:1 Nao Wamidiani wakamuuza huko Misri, kwa Potifa, mmoja wa maofisa wa Farao, mkuu wa askari walinzi.

Iliyochaguliwa sasa

Mwanzo 37: SRUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha