Mwanzo 3:6-16
Mwanzo 3:6-16 SRUV
Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alichuma matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala. Wakafumbuliwa macho wote wawili wakajitambua kuwa wako uchi, wakashona majani ya mtini, na kujifanyia mavazi ya kusitiri uchi wao. Kisha wakasikia sauti ya BWANA Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua kupunga; Adamu na mkewe wakajificha kati ya miti ya bustani, BWANA Mungu asiwaone. BWANA Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Akasema, Nilisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha. Akasema, Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je! Umekula matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala. BWANA Mungu akamwambia mwanamke, Nini hili ulilolifanya? Mwanamke akasema, Nyoka alinidanganya, nikala. BWANA Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako; nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino. Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa uchungu utazaa watoto; hata hivyo, hamu yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala.