Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 20:1-18

Mwanzo 20:1-18 SRUV

Abrahamu akaondoka huko kwenda nchi ya kusini, akakaa kati ya Kadeshi na Shuri, naye akatembea katika Gerari. Abrahamu akanena juu ya Sara mkewe, “Huyu ni dada yangu”. Basi Abimeleki mfalme wa Gerari akatuma watu wakamtwaa Sara. Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto ya usiku, akamwambia, Umekuwa mfu wewe kwa sababu ya mwanamke huyu uliyemtwaa, maana ni mke wa mtu. Basi Abimeleki alikuwa hakumkaribia, akasema, Ee Bwana, Je! Utaua hata taifa lenye haki? Je! Hukuniambia mwenyewe, “Huyu ni dada yangu?” Na mwanamke mwenyewe naye akasema, “Huyu ni kaka yangu”. Kwa ukamilifu wa moyo wangu, na kwa kutojua kwangu, nimefanya hivi. Mungu akamwambia katika ndoto, Nami nimejua ya kwamba kwa ukamilifu wa moyo wako umefanya hivi, ndipo nami nikakuzuia usinitendee dhambi, kwa hiyo sikukuacha umguse. Basi sasa umrudishe mwanamke kwa mtu huyo, maana yeye ni nabii, naye atakuombea, upate kuishi. Bali usipomrudisha, fahamu ya kwamba kwa hakika utakufa wewe na watu wote ulio nao. Abimeleki akaamka asubuhi na mapema, akawaita watumwa wake wote, akawaambia maneno hayo yote, nao watu hao wakaogopa sana. Kisha Abimeleki akamwita Abrahamu, akamwambia, Umetutenda nini? Nimekukosa nini, hata ukaleta juu yangu na juu ya ufalme wangu dhambi kuu? Umenitenda matendo yasiyotendeka. Abimeleki akamwambia Abrahamu, Umeona nini hata ukatenda jambo hili? Abrahamu akasema, Kwa kuwa niliona, hakika hapana hofu ya Mungu mahali hapa, nao wataniua kwa ajili ya mke wangu. Hata hivyo, kwa kweli yeye ni dada yangu, yaani binti wa baba yangu na wala sio binti wa mama yangu; ndipo akawa mke wangu. Ikawa hapo Mungu aliponisafirisha kutoka nyumba ya baba yangu, nikamwambia, Hii ndiyo fadhili yako, utakayonifanyia. Kila mahali tuingiapo, useme, Huyu ni kaka yangu. Basi Abimeleki akatwaa kondoo, na ng'ombe, na watumwa, na wajakazi, akampa Abrahamu, akamrudishia Sara mkewe. Abimeleki akasema, Nchi yangu iko mbele yako, ishi upendapo. Naye akamwambia Sara, Tazama! Nimempa ndugu yako fedha elfu moja, itakuwa kifunika macho kwako mbele ya wote walio pamoja nawe, nawe utakuwa na haki mbele ya watu wote. Abrahamu akamwomba Mungu, Mungu akamponya Abimeleki, na mkewe, na wajakazi wake, nao wakazaa wana. Maana BWANA alikuwa ameyafunga matumbo ya watu wa nyumbani mwa Abimeleki, wasizae, kwa ajili ya Sara mkewe Abrahamu.

Soma Mwanzo 20