Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 20:1-18

Mwanzo 20:1-18 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Basi Abrahamu akaendelea mbele kutoka huko hadi nchi ya Negebu na akaishi kati ya Kadeshi na Shuri. Kwa muda mfupi alikaa Gerari kama mgeni, huko Abrahamu akasema kuhusu Sara mkewe, “Huyu ni dada yangu.” Kisha Abimeleki mfalme wa Gerari akatuma Sara aletwe, naye akamchukua. Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto wakati wa usiku na kumwambia, “Wewe ni kama mfu kwa sababu ya huyu mwanamke uliyemchukua; yeye ni mke wa mtu.” Wakati huo Abimeleki alikuwa bado hajamsogelea, kwa hiyo akasema, “Je, Bwana utaliharibu taifa lisilo na hatia? Hakusema kwangu, ‘Huyu ni dada yangu,’ naye Sara pia hakusema, ‘Huyu ni kaka yangu’? Nimefanya haya kwa dhamiri njema na mikono safi.” Kisha Mungu akamwambia katika ndoto, “Ndiyo, najua ya kwamba umefanya haya kwa dhamiri safi, kwa hiyo nimekuzuia usinitende dhambi. Ndiyo sababu sikukuacha umguse. Sasa umrudishe huyo mke wa mtu, kwa maana ni nabii, naye atakuombea nawe utaishi. Lakini kama hutamrudisha, ujue kwa hakika kuwa wewe na watu wako wote mtakufa.” Kesho yake asubuhi na mapema Abimeleki akawaita maafisa wake wote, na baada ya kuwaambia yote yaliyotokea, waliogopa sana. Kisha Abimeleki akamwita Abrahamu na kumwambia, “Wewe umetufanyia nini? Nimekukosea nini hata ukaleta hatia kubwa namna hii juu yangu na ufalme wangu? Umenifanyia mambo ambayo hayakupasa kufanyika.” Abimeleki akamuuliza Abrahamu, “Ulikuwa na kusudi gani kufanya hivi?” Abrahamu akajibu, “Niliwaza kwamba, ‘Hakika hakuna hofu ya Mungu mahali hapa, nao wataniua kwa sababu ya mke wangu.’ Pamoja na hayo, ni kweli kwamba yeye ni dada yangu, binti wa baba yangu ingawa si mtoto wa mama yangu; basi akawa mke wangu. Wakati BWANA aliponifanya nisafiri mbali na nyumbani mwa baba yangu, nilimwambia, ‘Hivi ndivyo utakavyoonyesha pendo lako kwangu: Kila mahali tutakapokwenda, kuhusu mimi sema, “Huyu ni kaka yangu.” ’ ” Kisha Abimeleki akatwaa kondoo na ngʼombe, na watumwa wa kiume na wa kike akampa Abrahamu, akamrudisha Sara kwa mumewe. Abimeleki akasema, “Nchi yangu iko mbele yako, ishi popote unapotaka.” Akamwambia Sara, “Ninampa kaka yako shekeli elfu moja za fedha. Hii ni kufidia kosa lililofanyika dhidi yako mbele ya wote walio pamoja nawe; haki yako imethibitishwa kabisa.” Kisha Abrahamu akamwomba Mungu, naye Mungu akamponya Abimeleki, mke wake, na watumwa wake wa kike kwamba waweze kupata watoto tena, kwa kuwa BWANA alikuwa ameyafunga matumbo ya wote katika nyumba ya Abimeleki kwa sababu ya Sara, mke wa Abrahamu.

Shirikisha
Soma Mwanzo 20

Mwanzo 20:1-18 Biblia Habari Njema (BHN)

Toka Mamre, Abrahamu alisafiri kuelekea eneo la Negebu, akafanya makao yake kati ya Kadeshi na Shuri, kisha akaenda kukaa kwa muda huko Gerari. Akiwa huko, Abrahamu alisema kuwa mkewe Sara ni dada yake. Kwa hiyo, mfalme Abimeleki wa Gerari akamchukua Sara. Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto usiku, akamwambia, “Wewe utakufa kwa sababu ya mwanamke uliyemchukua, kwani ana mumewe.” Abimeleki ambaye bado hakuwa amelala na Sara, akajibu, “Bwana, utawaua watu wasio na hatia. Abrahamu mwenyewe ndiye aliyesema kuwa huyu ni dada yake. Tena hata Sara mwenyewe alisema kuwa Abrahamu ni kaka yake! Mimi nimefanya nilivyofanya kwa moyo mnyofu na sina hatia.” Basi, Mungu akamwambia katika hiyo ndoto, “Sawa. Najua kwamba umefanya hivyo kwa moyo mnyofu, na mimi ndiye niliyekuzuia kutenda dhambi dhidi yangu; ndiyo maana sikukuruhusu umguse huyo mwanamke. Sasa mrudishe huyo mwanamke kwa mume wake. Abrahamu ni nabii, naye atakuombea nawe utaishi. Lakini usipomrudisha, ujue kwa hakika kwamba wewe utakufa pamoja na watu wako wote.” Basi, Abimeleki akaamka asubuhi na mapema, akawaita watumishi wake wote na kuwaeleza mambo aliyoyaona katika ndoto; nao wakaogopa sana. Ndipo Abimeleki akamwita Abrahamu, akamwuliza, “Umetutendea nini? Nimekukosea nini hata ukaniletea balaa hili mimi na ufalme wangu? Umenitendea mambo yasiyostahili kutendwa.” Tena Abimeleki akazidi kumwuliza, “Ni kitu gani kimekusukuma kufanya hivyo?” Abrahamu akamjibu, “Nilifanya hivyo kwa kuwa hakuna amchaye Mungu mahali hapa, na kwamba mngeniua ili mumchukue mke wangu. Zaidi ya hayo, kwa kweli, yeye ni dada yangu: Baba yake na baba yangu ni mmoja, lakini mama tofauti; ndiyo maana akawa mke wangu. Wakati Mungu aliponifanya niiache nyumba ya baba yangu na kwenda ugenini, nilimwambia mke wangu, ‘Popote tutakapokwenda tafadhali useme kwamba mimi ni kaka yako!’” Abimeleki akamrudishia Abrahamu mke wake Sara, akampa na kondoo, ng'ombe na watumwa wa kiume na kike. Tena Abimeleki akamwambia Abrahamu, “Tazama, nchi hii yote ni yangu! Basi, chagua popote upendapo, ukae.” Kisha, akamwambia Sara, “Tazama, mimi nimempa ndugu yako vipande 1,000 vya fedha ili kuwaonesha wote walio pamoja nawe kwamba huna hatia; umethibitishwa huna lawama.” Kisha Abrahamu akamwomba Mungu, naye akamponya Abimeleki, mkewe na mjakazi wake, hata wakaweza kupata tena watoto. Hapo kwanza Mwenyezi-Mungu alikuwa amewazuia wanawake wote wa nyumba ya Abimeleki kupata watoto kwa sababu ya Sara, mke wa Abrahamu.

Shirikisha
Soma Mwanzo 20

Mwanzo 20:1-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Abrahamu akaondoka huko kwenda nchi ya kusini, akakaa kati ya Kadeshi na Shuri, naye akatembea katika Gerari. Abrahamu akanena juu ya Sara mkewe, “Huyu ni dada yangu”. Basi Abimeleki mfalme wa Gerari akatuma watu wakamtwaa Sara. Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto ya usiku, akamwambia, Umekuwa mfu wewe kwa sababu ya mwanamke huyu uliyemtwaa, maana ni mke wa mtu. Basi Abimeleki alikuwa hakumkaribia, akasema, Ee Bwana, Je! Utaua hata taifa lenye haki? Je! Hukuniambia mwenyewe, “Huyu ni dada yangu?” Na mwanamke mwenyewe naye akasema, “Huyu ni kaka yangu”. Kwa ukamilifu wa moyo wangu, na kwa kutojua kwangu, nimefanya hivi. Mungu akamwambia katika ndoto, Nami nimejua ya kwamba kwa ukamilifu wa moyo wako umefanya hivi, ndipo nami nikakuzuia usinitendee dhambi, kwa hiyo sikukuacha umguse. Basi sasa umrudishe mwanamke kwa mtu huyo, maana yeye ni nabii, naye atakuombea, upate kuishi. Bali usipomrudisha, fahamu ya kwamba kwa hakika utakufa wewe na watu wote ulio nao. Abimeleki akaamka asubuhi na mapema, akawaita watumwa wake wote, akawaambia maneno hayo yote, nao watu hao wakaogopa sana. Kisha Abimeleki akamwita Abrahamu, akamwambia, Umetutenda nini? Nimekukosa nini, hata ukaleta juu yangu na juu ya ufalme wangu dhambi kuu? Umenitenda matendo yasiyotendeka. Abimeleki akamwambia Abrahamu, Umeona nini hata ukatenda jambo hili? Abrahamu akasema, Kwa kuwa niliona, hakika hapana hofu ya Mungu mahali hapa, nao wataniua kwa ajili ya mke wangu. Hata hivyo, kwa kweli yeye ni dada yangu, yaani binti wa baba yangu na wala sio binti wa mama yangu; ndipo akawa mke wangu. Ikawa hapo Mungu aliponisafirisha kutoka nyumba ya baba yangu, nikamwambia, Hii ndiyo fadhili yako, utakayonifanyia. Kila mahali tuingiapo, useme, Huyu ni kaka yangu. Basi Abimeleki akatwaa kondoo, na ng'ombe, na watumwa, na wajakazi, akampa Abrahamu, akamrudishia Sara mkewe. Abimeleki akasema, Nchi yangu iko mbele yako, ishi upendapo. Naye akamwambia Sara, Tazama! Nimempa ndugu yako fedha elfu moja, itakuwa kifunika macho kwako mbele ya wote walio pamoja nawe, nawe utakuwa na haki mbele ya watu wote. Abrahamu akamwomba Mungu, Mungu akamponya Abimeleki, na mkewe, na wajakazi wake, nao wakazaa wana. Maana BWANA alikuwa ameyafunga matumbo ya watu wa nyumbani mwa Abimeleki, wasizae, kwa ajili ya Sara mkewe Abrahamu.

Shirikisha
Soma Mwanzo 20

Mwanzo 20:1-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ibrahimu akaondoka huko kwenda nchi ya kusini, akakaa kati ya Kadeshi na Shuri, naye akatembea katika Gerari. Ibrahimu akamnena Sara mkewe, Huyu ni ndugu yangu. Basi Abimeleki mfalme wa Gerari akapeleka watu akamtwaa Sara. Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto ya usiku, akamwambia, Umekuwa mfu wewe kwa sababu ya mwanamke huyu uliyemtwaa, maana ni mkewe mtu. Basi Abimeleki alikuwa hakumkaribia, akasema, Ee Bwana, Je! Utaua hata taifa lenye haki? Je! Hakuniambia mwenyewe, Huyu ni ndugu yangu? Na mwanamke mwenyewe naye alisema, Huyu ni ndugu yangu. Kwa ukamilifu wa moyo wangu, na kwa kuwa safi mikono yangu, nimefanya hivi. Mungu akamwambia katika ndoto, Nami nimejua ya kwamba kwa ukamilifu wa moyo wako umefanya hivi, ndipo nami nikakuzuia usinitendee dhambi, kwa hiyo sikukuacha umguse. Basi sasa umrudishe mwanamke kwa mtu huyo, maana yeye ni nabii, naye atakuombea, upate kuishi. Bali usipomrudisha, fahamu ya kwamba kwa hakika utakufa wewe na watu wote ulio nao. Abimeleki akaamka asubuhi na mapema, akawaita watumwa wake wote, akawaambia maneno hayo yote masikioni mwao, nao watu hao wakaogopa sana. Kisha Abimeleki akamwita Ibrahimu, akamwambia, Umetutenda nini? Nimekukosa nini, hata ukaleta juu yangu na juu ya ufalme wangu dhambi kuu? Umenitenda matendo yasiyotendeka. Abimeleki akamwambia Ibrahimu, Umeona nini hata ukatenda jambo hili? Ibrahimu akasema, Kwa sababu naliona, Yakini hapana hofu ya Mungu mahali hapa, nao wataniua kwa ajili ya mke wangu. Naye kweli ni ndugu yangu, binti wa baba yangu ila siye mwana wa mama yangu, ndipo akawa mke wangu. Ikawa hapo Mungu aliponisafirisha kutoka nyumba ya baba yangu, nikamwambia, Hii ndiyo fadhili yako, utakayonifanyia. Kila mahali tuingiapo, useme, Huyu ni ndugu yangu. Basi Abimeleki akatwaa kondoo, na ng’ombe, na watumwa, na wajakazi, akampa Ibrahimu, akamrudishia Sara mkewe. Abimeleki akasema, Nchi yangu iko mbele yako, kaa upendapo. Naye akamwambia Sara, Tazama! Nimempa ndugu yako fedha elfu, itakuwa kifunika macho kwako mbele ya wote walio pamoja nawe, nawe utakuwa na haki mbele ya watu wote. Ibrahimu akamwomba Mungu, Mungu akamponya Abimeleki, na mkewe, na wajakazi wake, nao wakazaa wana. Maana BWANA alikuwa ameyafunga matumbo ya watu wa nyumbani mwa Abimeleki, wasizae, kwa ajili ya Sara mkewe Ibrahimu.

Shirikisha
Soma Mwanzo 20