Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 13:1-13

Mwanzo 13:1-13 SRUV

Abramu akapanda kutoka Misri, yeye, na mkewe, na kila alichokuwa nacho, na Lutu pamoja naye, mpaka kusini. Naye Abramu alikuwa tajiri sana kwa mifugo, kwa fedha, na kwa dhahabu. Akaendelea kusafiri kutoka kusini mpaka Betheli, mahali pale palipokuwapo hema yake kwanza, kati ya Betheli na Ai; napo ndipo palipokuwa na madhabahu aliyofanya hapo kwanza; naye Abramu akaliitia jina la BWANA hapo. Na Lutu aliyesafiri pamoja na Abramu, yeye naye alikuwa na makundi ya ng'ombe na kondoo, na hema. Na ile nchi haikuwatosha, ili wakae pamoja; maana mali zao zilikuwa nyingi, hata wasiweze kukaa pamoja. Kukawako ugomvi kati ya wachunga wanyama wa Abramu, na wachunga wanyama wa Lutu; na siku zile Wakanaani na Waperizi walikuwa wakikaa katika nchi. Abramu akamwambia Lutu, Basi, usiwepo ugomvi, nakusihi, kati yangu na wewe, wala kati ya wachungaji wangu na wachungaji wako; maana sisi tu jamaa moja. Je! Nchi hii yote haiko mbele yako? Basi jitenge nami, nakusihi; ukienda upande wa kushoto, nitakwenda upande wa kulia; ukienda upande wa kulia, nitakwenda upande wa kushoto. Lutu akainua macho yake, akaliona Bonde lote la Yordani, ya kwamba lote pia lina maji, kabla BWANA hajaharibu Sodoma na Gomora, lilikuwa kama bustani ya BWANA, kama nchi ya Misri hapo unapokwenda Soari. Basi Lutu akajichagulia Bonde lote la Yordani; Lutu akasafiri kwenda upande wa mashariki; wakatengana wao kwa wao. Abramu akakaa katika nchi ya Kanaani, na Lutu akakaa katika miji ya lile Bonde; akajongeza hema yake mpaka Sodoma. Lakini watu wa Sodoma walikuwa wabaya, wenye kufanya dhambi nyingi sana juu ya BWANA.

Soma Mwanzo 13

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Mwanzo 13:1-13