Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 1:9-26

Mwanzo 1:9-26 SRUV

Mungu akasema, Maji yaliyo chini ya mbingu na yakusanyike mahali pamoja, ili pakavu paonekane; ikawa hivyo. Mungu akapaita pale pakavu Nchi; na makusanyiko ya maji akayaita Bahari; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Mungu akasema, Nchi na itoe majani, mimea itoayo mbegu, na miti ya matunda izaayo matunda kwa jinsi yake, ambao mbegu zake zimo ndani yake, juu ya nchi; ikawa hivyo. Nchi ikatoa majani, mche utoao mbegu kwa jinsi yake, na mti uzaao matunda, ambao mbegu zake zimo ndani yake, kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya tatu. Mungu akasema, Na iwe mianga katika anga la mbingu ili itenge kati ya mchana na usiku; nayo iwe ndiyo dalili ya kuonesha majira, siku na miaka; tena iwe ndiyo mianga katika anga la mbingu itie nuru juu ya nchi; ikawa hivyo. Mungu akaumba mianga miwili mikubwa, ule mkubwa utawale mchana, na ule mdogo utawale usiku; akafanya na nyota pia. Mungu akaiweka katika anga la mbingu, itie nuru juu ya nchi na kuutawala mchana na usiku na kutenga nuru na giza; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya nne. Mungu akasema, Maji na yajawe kwa wingi na viumbe vyenye uhai, na ndege waruke juu ya nchi katika anga la mbingu. Mungu akaumba nyangumi wakubwa, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho, ambavyo maji yalijawa navyo kwa wingi kwa jinsi zao, na kila ndege arukaye, kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Mungu akavibarikia, akisema, Zaeni, mkaongezeke, mkayajaze maji ya baharini, ndege na wazidi katika nchi. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya tano. Mungu akasema, Nchi na izae kiumbe hai kwa jinsi zake, mnyama wa kufugwa, nacho kitambaacho, na wanyama wa mwitu kwa jinsi zake; ikawa hivyo. Mungu akaumba aina zote za wanyama wa porini na wa kufugwa na viumbe vyote vitambaavyo nchini; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila kiumbe kitambaacho nchini.

Soma Mwanzo 1

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Mwanzo 1:9-26