Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Wagalatia 2:1-21

Wagalatia 2:1-21 SRUV

Kisha, baada ya miaka kumi na minne, nilipanda tena kwenda Yerusalemu pamoja na Barnaba, nikamchukua na Tito pamoja nami. Nami nilikwenda kwa kuwa nilifunuliwa, nikawaeleza Injili ile niihubiriyo katika Mataifa, lakini kwa faragha kwa hao viongozi waliosifika, isiwe labda napiga mbio bure, au nilipiga mbio bure. Lakini Tito aliyekuwa pamoja nami, naye ni Mgiriki, hakulazimishwa kutahiriwa. Bali kwa ajili ya ndugu za uongo walioingizwa kwa siri; ambao waliingia kwa siri ili kuupeleleza uhuru wetu tulio nao katika Kristo Yesu, ili watutie utumwani; ambao hata saa moja hatukujitia chini yao, ili kwamba kweli ya Injili ikae pamoja nanyi. Lakini wale viongozi waliosifika kuwa wana cheo; (walivyokuwa vyovyote ni mamoja kwangu; Mungu hapokei uso wa mwanadamu); nasema, hao waliosifika hawakuniongezea kitu; bali, kinyume cha hayo, walipoona ya kuwa nimekabidhiwa Injili ya wasiotahiriwa, kama vile Petro alivyokabidhiwa ya waliotahiriwa; (maana yeye aliyemwezesha Petro kuwa mtume wa waliotahiriwa ndiye aliyeniwezesha mimi kwenda kwa Mataifa); tena Yakobo, Kefa, na Yohana, waliosifika kuwa ni nguzo, walipoitambua ile neema niliyopewa, walinipa mimi na Barnaba mkono wa kulia wa kuonesha ushirikiano; ili sisi tuende kwa Mataifa, na wao waende kwa watu wa tohara; ila neno moja tu walitutakia, tuwakumbuke maskini; nami neno lilo hilo nilikuwa na bidii kulifanya. Lakini Kefa alipokuja Antiokia, nilishindana naye uso kwa uso, kwa sababu alistahili hukumu. Kwa maana kabla hawajaja watu kadhaa waliotoka kwa Yakobo, alikuwa akila pamoja na watu wa Mataifa; lakini hao walipokuja, akarudi nyuma akajitenga, huku akiwaogopa waliotahiriwa. Na hao Wayahudi wengine wakajigeuza pamoja naye, hata na Barnaba pia akachukuliwa na unafiki wao. Lakini, nilipoona ya kuwa njia yao haiendi sawasawa na ile kweli ya Injili, nilimwambia Kefa mbele ya wote, Ikiwa wewe uliye Myahudi wafuata desturi za Mataifa, wala si za Wayahudi, kwa nini unawashurutisha Mataifa kufuata desturi za Wayahudi? Sisi tulio Wayahudi kwa asili, wala si wa Mataifa wenye dhambi, Lakini tukijua ya kuwa mwanadamu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria, bali kwa imani ya Kristo Yesu; sisi tulimwamini Kristo Yesu ili tuhesabiwe haki kwa imani ya Kristo, wala si kwa matendo ya sheria; maana kwa matendo ya sheria hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki. Lakini ikiwa sisi wenyewe, kwa kutafuta kuhesabiwa haki katika Kristo, tulionekana kuwa wenye dhambi, je! Kristo amekuwa mtumishi wa dhambi? La hasha! Maana nikiyajenga tena yale niliyoyabomoa, naonesha ya kuwa mimi mwenyewe ni mkosaji. Maana mimi kwa njia ya sheria niliifia sheria ili nimwishie Mungu. Nimesulubiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu. Siibatili neema ya Mungu; maana, ikiwa haki hupatikana kwa njia ya sheria, basi Kristo alikufa bure.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Wagalatia 2:1-21