Ezra 7:11-28
Ezra 7:11-28 SRUV
Basi hii ndiyo nakala ya barua, ambayo mfalme Artashasta alimpa Ezra, kuhani, mwandishi, mjuzi wa amri za BWANA, na sheria zake alizowapa Waisraeli. Artashasta, mfalme wa wafalme, kwa Ezra, kuhani, mwandishi wa Torati ya Mungu wa mbinguni, wasalamu; na kadhalika. Natoa amri ya kwamba watu wote walio wa Israeli, na makuhani wao, na Walawi, katika ufalme wangu, wenye nia ya kwenda Yerusalemu kwa hiari yao wenyewe, waende pamoja nawe. Kwa kuwa umetumwa na mfalme, na washauri wake saba, ili kuuliza habari za Yuda na Yerusalemu, kwa sheria ya Mungu wako iliyo mkononi mwako; na kuichukua fedha na dhahabu, ambayo mfalme, na washauri wake, kwa hiari yao, wamemtolea Mungu wa Israeli, akaaye Yerusalemu; na fedha yote na dhahabu utakayoona katika wilaya ya Babeli, pamoja na vitu watakavyotoa watu kwa hiari yao, na vitu vya makuhani walivyotoa kwa hiari yao, kwa ajili ya nyumba ya Mungu wao iliyoko Yerusalemu. Kwa sababu hiyo ujitahidi kununua kwa fedha hiyo mafahali, kondoo dume, wana-kondoo, pamoja na sadaka zao za unga, na sadaka zao za kinywaji; nawe utazitoa juu ya madhabahu ya nyumba ya Mungu wenu, iliyoko Yerusalemu. Na jambo lolote mtakaloona vema kulitenda, wewe na ndugu zako, kwa ile fedha na dhahabu itakayobaki, hilo litendeni, kama apendavyo Mungu wenu. Na vile vyombo upewavyo kwa huduma ya nyumba ya Mungu wako, virejeshe mbele za Mungu wa Yerusalemu. Na chochote kitakachohitajiwa zaidi, kwa ajili ya nyumba ya Mungu wako, kitakachokupasa kukitoa, kitoe katika nyumba ya hazina ya mfalme. Na mimi, naam mimi, mfalme Artashasta, nawapa amri watunza hazina wote, walio ng'ambo ya Mto, ya kwamba, kila neno ambalo Ezra, kuhani, mwandishi wa Torati ya Mungu wa mbinguni, atalitaka kwenu, na litendeke kwa bidii nyingi, hata kiasi cha talanta mia moja za fedha, na vipimo mia vya ngano, na bathi mia moja za divai, na bathi mia moja za mafuta na chumvi ya kiasi chochote kile. Kila neno litakaloamriwa na Mungu wa mbinguni, na litendeke kikamilifu kwa ajili ya nyumba ya Mungu wa mbinguni. Kwa nini itokee ghadhabu juu ya ufalme wa mfalme na wanawe? Tena tunawaarifu ya kuwa katika habari ya makuhani, na Walawi, na waimbaji, na mabawabu na Wanethini, au watumishi wa nyumba hii ya Mungu, si halali kuwatoza kodi, wala ada, wala ushuru. Na wewe, Ezra, kwa kadiri ya hekima ya Mungu wako iliyo mkononi mwako, waweke mahakimu na majaji, watakaowaamua watu wote walio ng'ambo ya Mto, yaani, wote wenye kuzijua amri za Mungu wako; na ukamfundishe yeye asiyezijua. Na kila mtu asiyekubali kuitenda sheria ya Mungu wako, na sheria ya mfalme, na apatilizwe hukumu kali, iwe ni kuuawa, au ni kuhamishwa, au kunyang'anywa mali yake, au kufungwa. Na ahimidiwe BWANA, Mungu wa baba zetu, aliyetia neno kama hilo katika moyo wa mfalme, kuipamba nyumba ya BWANA iliyoko Yerusalemu. Naye amenifikishia rehema zake mbele ya mfalme, na washauri wake, na mbele ya wakuu wote wa mfalme wenye mamlaka. Nami nikatiwa nguvu, kwa kadiri mkono wa BWANA, Mungu wangu, ulivyokuwa pamoja nami, nikawakusanya wakuu wote katika Israeli, ili wakwee pamoja nami.