Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezra 4:6-24

Ezra 4:6-24 SRUV

Tena, wakati wa kutawala kwake Ahasuero, mwanzo wa kutawala kwake, watu wakaandika mashitaka juu ya wenyeji wa Yuda na Yerusalemu. Na tena, katika siku za Artashasta, Mithredathi, na Tabeeli na wenzao wengine, wakimwandikia Artashasta, mfalme wa Uajemi, salamu za heri; na mwandiko wa waraka huo, ukaandikwa kwa herufi za Kiaramu, na kusomwa kwa lugha ya Kiaramu. Nao Rehumu, mtawala, na Shimshai, mwandishi, wakaandika waraka juu ya Yerusalemu kwa Artashasta, mfalme, kama hivi; Rehumu, mtawala, na Shimshai, mwandishi, na wenzao wengine, makadhi wa Kiajemi na madiwani wa Kiajemi; na Waarkewi, Wababeli, Washushani, yaani, Waelami; na watu wengine wa mataifa, ambao Asur-bani-pali mkuu, mwenye heshima, aliwavusha, na kuwakalisha katika mji wa Samaria, na mahali penginepo, ng'ambo ya Mto; na kadhalika. Hii ndiyo nakala ya waraka waliyompelekea mfalme Artashasta; Watumishi wako, watu walio ng'ambo ya Mto; wakadhalika. Ijulikane kwa mfalme ya kuwa Wayahudi, waliokwea kutoka kwako, wamefika kwetu Yerusalemu; nao wanaujenga ule mji mwasi, mbaya; wamemaliza kuta zake, na kuitengeneza misingi yake. Basi, ijulikane kwa mfalme, ya kuwa mji huu ukijengwa, na kuta zake zikimalizika, hawatatoa kodi, wala ada, wala ushuru, na mwisho wake wafalme watapata hasara. Na sisi, kwa kuwa tunakula chumvi ya nyumba ya mfalme, wala si wajibu wetu kumwona mfalme akivunjiwa heshima, basi tumetuma watu na kumwarifu mfalme. Ili habari zichunguzwe katika kitabu cha kumbukumbu za baba zako; ndivyo utakavyopata kujua kwa kitabu cha kumbukumbu ya kuwa mji huo ni mji mwasi, wenye kuwadhuru wafalme, na wakuu wa mikoa, na ya kuwa wenyeji wake wamefanya fitina katika mji huo zamani; ndiyo sababu mji huo ukaangamizwa. Tunamwarifu mfalme ya kuwa mji huo ukijengwa, na kuta zake zikimalizika, basi utakuwa huna milki katika sehemu ya nchi iliyo ng'ambo ya mto. Ndipo mfalme akatuma majibu; Kwa Rehumu, mtawala, na Shimshai, mwandishi, na wenzao wengine waliokaa katika Samaria, na penginepo ng'ambo ya Mto, Salamu; na kadhalika. Ule barua mliotutumia umesomwa wazi mbele yangu, nami nikaielewa. Nikatoa amri, na watu wametafuta habari; ikaonekana ya kuwa mji huu zamani umewaasi wafalme, na ya kuwa uasi na fitina zimefanyika ndani yake. Tena walikuwako wafalme wakuu juu ya Yerusalemu, waliotawala nchi yote iliyo ng'ambo ya Mto; wakapewa kodi, na ada, na ushuru. Sasa toeni amri kuwakomesha watu hawa kazi yao, mji huu usijengwe, hadi nitakapotoa amri. Tena jihadharini, msilegee katika jambo hili; kwa nini madhara yazidi, na wafalme wapate hasara? Kisha nakala ya barua hiyo ya mfalme Artashasta iliposomwa mbele ya Rehumu, mtawala na Shimshai, mwandishi, na wenzao, wakaenda Yerusalemu upesi, kwa Wayahudi, wakawakomesha kwa nguvu na kwa kuwashurutisha. Hivyo kazi ya nyumba ya Mungu iliyoko Yerusalemu ikakoma; nayo ikakoma hadi mwaka wa pili wa kutawala kwake Dario, mfalme wa Uajemi.

Soma Ezra 4

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Ezra 4:6-24

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha