Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezra 4:1-16

Ezra 4:1-16 SRUV

Basi adui za Yuda na Benyamini, waliposikia ya kuwa wana wa uhamisho wanamjengea BWANA, Mungu wa Israeli, hekalu, wakamkaribia Zerubabeli, na wakuu wa koo za mababa, wakawaambia, Na tujenge sisi nasi pamoja nanyi; kwa maana tunamtafuta Mungu wenu kama ninyi, nasi tumemtolea dhabihu tangu zamani za Esar-hadoni, mfalme wa Ashuru, aliyetupandisha mpaka hapa. Lakini Zerubabeli, na Yoshua, na wakuu wengine wa koo za mababa katika Israeli, wakawaambia, Ninyi haiwahusu kushirikiana nasi katika kumjengea Mungu wetu nyumba; bali sisi wenyewe peke yetu tutamjengea BWANA, Mungu wa Israeli, nyumba, kama mfalme Koreshi, mfalme wa Uajemi, alivyotuamuru. Ndipo wakazi wa nchi wakawavunja moyo watu wa Yuda, wakawafanya wawe na hofu ya kujenga. Wakawahonga maofisa, ili kuwakatisha tamaa katika mpango wao, siku zote za Koreshi, mfalme wa Uajemi, hata wakati wa kutawala kwake Dario, mfalme wa Uajemi. Tena, wakati wa kutawala kwake Ahasuero, mwanzo wa kutawala kwake, watu wakaandika mashitaka juu ya wenyeji wa Yuda na Yerusalemu. Na tena, katika siku za Artashasta, Mithredathi, na Tabeeli na wenzao wengine, wakimwandikia Artashasta, mfalme wa Uajemi, salamu za heri; na mwandiko wa waraka huo, ukaandikwa kwa herufi za Kiaramu, na kusomwa kwa lugha ya Kiaramu. Nao Rehumu, mtawala, na Shimshai, mwandishi, wakaandika waraka juu ya Yerusalemu kwa Artashasta, mfalme, kama hivi; Rehumu, mtawala, na Shimshai, mwandishi, na wenzao wengine, makadhi wa Kiajemi na madiwani wa Kiajemi; na Waarkewi, Wababeli, Washushani, yaani, Waelami; na watu wengine wa mataifa, ambao Asur-bani-pali mkuu, mwenye heshima, aliwavusha, na kuwakalisha katika mji wa Samaria, na mahali penginepo, ng'ambo ya Mto; na kadhalika. Hii ndiyo nakala ya waraka waliyompelekea mfalme Artashasta; Watumishi wako, watu walio ng'ambo ya Mto; wakadhalika. Ijulikane kwa mfalme ya kuwa Wayahudi, waliokwea kutoka kwako, wamefika kwetu Yerusalemu; nao wanaujenga ule mji mwasi, mbaya; wamemaliza kuta zake, na kuitengeneza misingi yake. Basi, ijulikane kwa mfalme, ya kuwa mji huu ukijengwa, na kuta zake zikimalizika, hawatatoa kodi, wala ada, wala ushuru, na mwisho wake wafalme watapata hasara. Na sisi, kwa kuwa tunakula chumvi ya nyumba ya mfalme, wala si wajibu wetu kumwona mfalme akivunjiwa heshima, basi tumetuma watu na kumwarifu mfalme. Ili habari zichunguzwe katika kitabu cha kumbukumbu za baba zako; ndivyo utakavyopata kujua kwa kitabu cha kumbukumbu ya kuwa mji huo ni mji mwasi, wenye kuwadhuru wafalme, na wakuu wa mikoa, na ya kuwa wenyeji wake wamefanya fitina katika mji huo zamani; ndiyo sababu mji huo ukaangamizwa. Tunamwarifu mfalme ya kuwa mji huo ukijengwa, na kuta zake zikimalizika, basi utakuwa huna milki katika sehemu ya nchi iliyo ng'ambo ya mto.

Soma Ezra 4