Ezekieli 42:1-20
Ezekieli 42:1-20 SRUV
Ndipo akanileta mpaka ua wa nje, njia ya kuelekea upande wa kaskazini; akaniingiza katika chumba kilichopakabili mahali palipotengeka, na kilicholikabili jengo upande wa kaskazini; kukabili urefu wa dhiraa mia moja palikuwa na mlango wa kaskazini, na upana wake ni dhiraa hamsini. Kukabili zile dhiraa ishirini za ua wa ndani, na kukabili sakafu ya mawe ya ua wa nje, palikuwa na baraza kukabili baraza katika ghorofa ya tatu. Na mbele ya vile vyumba palikuwa na njia, upana wake dhiraa kumi upande wa ndani, njia ya dhiraa mia moja, na milango yake ilielekea upande wa kaskazini. Basi vile vyumba vya juu vilikuwa vifupi zaidi; kwa maana baraza zile zilivipunguza kuliko zilivyovipunguza vya chini na vya katikati. Maana vilikuwa vina ghorofa tatu, wala havikuwa na nguzo kama nguzo za zile nyua; basi kila kilichokuwa cha juu kilikuwa chembamba kuliko cha chini na cha katikati, kutoka chini. Na ukuta ule uliokuwa nje, ubavuni mwa vyumba vile, ulioelekea ua wa nje, kuvikabili vyumba vile, urefu wake ni dhiraa hamsini. Maana urefu wa vyumba vile, vilivyokuwa katika ua wa nje, ulikuwa dhiraa hamsini; na tazama, mbele ya hekalu, dhiraa mia moja. Na toka chini ya vyumba vile palikuwa na mahali pa kuingilia upande wa mashariki, mtu aviingiavyo toka ua wa nje. Tena palikuwa na vyumba katika unene wa ukuta wa ua, kuukabili upande wa mashariki, kupaelekea mahali palipotengeka, na kulielekea jengo. Nayo njia ilikuwa mbele yake, kuonekana kwake kulikuwa kama kuonekana kwake vyumba vile vilivyokuwa upande wa kaskazini, urefu ule ule, na upana ule ule; na mahali pake pa kutokea palikuwa sawasawa na vipimo vyake, na sawasawa na milango yake. Na sawasawa na milango ya vyumba, vilivyoelekea upande wa kusini, palikuwa na mlango katika mwisho wa njia ile; yaani, njia iliyoukabili ukuta upande wa mashariki, mtu akiingia. Kisha akaniambia, Vyumba vya upande wa kaskazini, na vyumba vya upande wa kusini, ambavyo vyaelekea mahali palipotengeka, ni vyumba vitakatifu; humo makuhani, wamkaribiao BWANA, watakula vitu vilivyo vitakatifu sana; humo wataviweka vitu vilivyo vitakatifu sana, na sadaka ya unga, na sadaka ya dhambi, na sadaka ya hatia; kwa maana mahali hapo ni patakatifu. Makuhani watakapoingia ndani, hawatatoka mahali patakatifu kwenda hadi katika ua wa nje; lakini wataweka mavazi yao katika mahali wahudumiapo; maana ni matakatifu; nao watavaa mavazi mengine, na kupakaribia mahali pa wazi kwa watu. Basi, alipokuwa amekwisha kuipima nyumba ya ndani, akanileta nje, kwa njia ya lango lililokabili upande wa mashariki, akalipima pande zote. Akaupima upande wa mashariki kwa mwanzi wa kupimia, mianzi mia tano, kwa mwanzi wa kupimia pande zote. Akaupima upande wa kaskazini, mianzi mia tano, kwa mwanzi wa kupimia pande zote. Akaupima upande wa kusini, mianzi mia tano, kwa mwanzi wa kupimia. Akageuka aelekee upande wa magharibi, akapima mianzi mia tano, kwa mwanzi wa kupimia. Alipima pande zake zote nne; lilikuwa na ukuta pande zote, urefu wake mianzi mia tano, na upana wake mianzi mia tano, ili kupatenga mahali palipo patakatifu, na mahali ambapo ni pa watu wote.