Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Esta 9:1-16

Esta 9:1-16 SRUV

Hata ulipofika mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari, siku yake ya kumi na tatu, amri ya mfalme na mbiu yake ilipowadia kutekelezwa; ambayo siku ile adui za Wayahudi walitumaini kuwatawala, bali kumebadilika kinyume, hata Wayahudi waliwatawala wale waliowachukia; siku ile ile Wayahudi wakakusanyika mijini mwao katika mikoa yote ya mfalme Ahasuero ili kuwatia mikono wale watu waliowatakia hasara; wala asiweze mtu kuwazuia, kwa kuwa waogopwa na watu wote. Nao wakuu wa mikoa, na majumbe, na watawala, na wale waliofanya shughuli ya mfalme, waliwasaidia Wayahudi; maana walimwogopa Mordekai. Maana Mordekai alikuwa mkuu nyumbani mwa mfalme, na sifa yake imevuma katika mikoa yote, kwa kuwa huyo Mordekai amezidi kukuzwa. Basi Wayahudi wakawapiga adui zao wote mapigo ya upanga, na kuwachinja, na kuwaangamiza, wakawatenda kama wapendavyo wale waliowachukia. Hata huko Susa mjini Wayahudi wakawaua watu mia tano, na kuwaangamiza. Wakawaua na Parshandatha, na Dalfoni, na Aspatha, na Poratha, na Adalia, na Aridatha, na Parmashta, na Arisai, na Aridai, na Waizatha, wana kumi wa Hamani mwana wa Hamedatha, adui ya Wayahudi; lakini juu ya nyara hawakuweka mikono. Siku ile mfalme akaletewa hesabu ya hao waliouawa huko Susa mjini. Mfalme akamwambia malkia Esta, Wayahudi wamewaua watu mia tano hapa Shushani ngomeni na kuwaangamiza, pamoja na wana kumi wa Hamani, je! Wamefanyaje basi katika majimbo ya mfalme yaliyosalia! Basi, una nini uombalo? Nawe utapewa; ama unayo haja gani tena? Nayo itatimizwa. Ndipo Esta aliposema, Mfalme akiona vema, Wayahudi walioko Susa na wapewe ruhusa kufanya tena kesho sawasawa na mbiu ya leo, na hao wana kumi wa Hamani watundikwe juu ya mti ule. Mfalme akaamuru ifanyike vivyo hivyo, mbiu ikapigwa huko Susa, wakawatundika wale wana kumi wa Hamani. Basi Wayahudi wa Susa wakakusanyika tena siku ya kumi na nne pia ya mwezi wa Adari, wakawaua watu mia tatu huko Susa; lakini juu ya nyara hawakuweka mikono. Nao Wayahudi wengine waliokaa katika mikoa ya mfalme walikusanyika, wakayapigania maisha yao, wakajipatia raha mbele ya adui zao, wakawaua waliowachukia, watu elfu sabini na tano; lakini juu ya nyara hawakuweka mikono.

Soma Esta 9