Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Esta 1:1-12

Esta 1:1-12 SRUV

Katika nyakati za Ahasuero; Ahasuero aliyetawala mikoa mia moja ishirini na saba, kutoka India mpaka Kushi; siku zile mfalme Ahasuero alipoketi katika kiti cha enzi cha ufalme wake, huko Susa, mji mkuu ngomeni; mwaka wa tatu wa kutawala kwake, ikawa aliwafanyia karamu wakuu na mawaziri wake; wakuu wa majeshi ya Uajemi na Umedi; watu maarufu na wakuu wa mikoa, wakihudhuria mbele zake. Akawaonesha utajiri wa ufalme wake mtukufu, na heshima ya enzi yake bora siku nyingi, yaani siku mia moja na themanini. Hata siku hizo zilipotimia, mfalme akawafanyia karamu watu wote waliokuwapo huko Shushani mji mkuu, wakubwa kwa wadogo, muda wa siku saba, katika ukumbi wa bustani ya ngome ya mfalme. Palikuwa na mapazia ya bafta, nyeupe na samawati, yamefungiwa kamba za kitani safi za rangi ya zambarau kwa pete za fedha na nguzo za marumaru; pia na vitanda vilikuwa vya dhahabu na fedha juu ya sakafu yenye nakshi ya vito vyekundu, marumaru, lulu za manjano na nyeusi na mawe ya thamani. Wakawanywesha kileo katika vyombo mbalimbali vya dhahabu, na divai tele ya kifalme, kufuatana na ukarimu wa ufalme; Walikunywa kama ilivyoamriwa, bila kushurutishwa; maana mfalme aliwaagiza watumishi wahudumie kila mtu kadiri ya mahitaji yake. Naye Vashti, malkia, akawafanyia karamu wanawake ndani ya nyumba ya kifalme ya mfalme Ahasuero. Katika siku ya saba, mfalme alipofurahiwa moyo wake kwa divai, aliwaamuru Mehumani, Biztha, Harbona, Bigtha, Abagtha, Zethari, na Karkasi, wale Matowashi saba, wasimamizi wa nyumba saba waliohudumu mbele zake, wamlete Vashti, malkia, mbele ya mfalme, akiwa amevaa taji la kifalme; ili kuwaonesha watu na wakuu uzuri wake, maana alikuwa mzuri wa uso. Bali Vashti, malkia, hakutii amri ya mfalme, alikataa kuja kama alivyoamriwa na mfalme kupitia kwa matowashi; kwa hiyo mfalme akaghadhibika sana, na hasira yake ikawaka ndani yake.

Soma Esta 1

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Esta 1:1-12