Danieli 11
11
1 #
Dan 9:1; 5:31 Kwa upande wangu, katika mwaka wa kwanza wa Dario, Mmedi, mimi nilisimama ili kumsaidia na kumtia nguvu.
2Nami sasa nitakuonesha yaliyo kweli. Tazama, watasimama wafalme watatu katika Uajemi; naye mfalme wa nne atakuwa tajiri kuliko hao wote; naye atakapopata nguvu kwa utajiri wake, atawachochea wote juu ya ufalme wa Ugiriki. 3#Dan 7:6; 8:4,5 Na mfalme hodari atasimama, atakayetawala kwa uwezo mkuu, na kutenda apendavyo. 4#Dan 7:8; 8:8,22; Mt 12:25 Naye atakaposimama, ufalme wake utavunjika, na kugawanyika katika pepo nne za mbinguni; lakini hautakuwa wa uzao wake, wala hautakuwa kama mamlaka yake ambayo alitawala kwayo; kwa maana ufalme wake utang'olewa, hata kwa ajili ya wengine zaidi ya hao.
5Na mfalme wa kusini atakuwa na nguvu; lakini mmoja wa maofisa wake atakuwa na nguvu zaidi kuliko yeye, na atatawala; himaya kubwa zaidi kuliko yeye. 6Na baada ya miaka kadhaa watashirikiana; kwa kuwa binti wa mfalme wa kusini atakuja kwa mfalme wa kaskazini, ili kufanya mapatano naye; lakini hatakuwa na nguvu za mkono wake sikuzote; wala mfalme yule hatasimama, wala mkono wake; lakini yule binti atatolewa, na hao waliomleta, na yeye aliyemzaa, na yeye aliyemtia nguvu, zamani zile. 7Lakini katika chipukizi la mizizi yake atasimama mmoja mahali pake atakayeliendesha jeshi la askari, naye ataingia katika ngome ya mfalme wa kaskazini, na kuwatenda mambo, na kuwashinda; 8na miungu yao, pamoja na sanamu zao, na vyombo vyao vizuri vya fedha na dhahabu atavichukua mpaka Misri; kisha atajizuia miaka kadhaa asimwendee mfalme wa kaskazini. 9Naye huyo ataingia katika ufalme wa mfalme wa kusini, lakini atarudi mpaka nchi yake mwenyewe. 10#Isa 8:8; Yer 46:7,8; Dan 9:26 Na wanawe watafanya vita, na kukusanya mkutano wa majeshi makuu; watakaokuja na kufurika na kupita katikati; nao watarudi na kufanya vita mpaka penye ngome yake. 11Na mfalme wa kusini ataingiliwa na ghadhabu, naye atatoka na kupigana naye, yaani, na mfalme wa kaskazini; naye atapanga jeshi kubwa; na jeshi hilo litawekwa mikononi mwake. 12#2 Nya 25:19; Mit 16:18; Isa 10:7-13; Dan 5:19,20 Atakapokwisha kuchukua lile jeshi, moyo wake utatukuzwa; naye atawaangusha makumi ya maelfu; lakini hataongezewa nguvu. 13Kwa maana mfalme wa kaskazini atarudi, naye atapanga jeshi kubwa kuliko lile la kwanza; naye hakika atakuja mwisho wa zamani zile, yaani, baada ya miaka kadhaa, pamoja na jeshi kubwa na mali nyingi. 14Na zamani zile watu wengi watasimama ili kumpinga mfalme wa kusini; pia, wenye jeuri miongoni mwa watu wako watajiinua ili kuyathibitisha maono; lakini wataanguka. 15#Yer 6:6; Zab 33:16 Basi mfalme wa kaskazini atakuja, na kufanya kilima, na kuupiga mji wenye maboma; na silaha za kusini hazitaweza kumpinga, wala watu wake wateule, wala hapatakuwa na nguvu za kumpinga. 16#Yos 1:5 Maana ajaye kupigana naye atatenda kadiri apendavyo, wala hapana mtu atakayesimama mbele yake; naye atasimama katika nchi ya uzuri, na uharibifu utakuwa mkononi mwake. 17#2 Nya 20:3; Dan 9:26 Naye atakaza uso wake ili aje pamoja na nguvu zote za ufalme wake, naye atafanya mapatano naye; naye atatenda kadiri apendavyo; naye atampa binti amuoe, ili hatimaye amwangamize huyo mfalme; lakini hataweza kumwangamiza. 18Baada ya hayo atauelekeza uso wake kwenye visiwa, naye atavipiga visiwa vingi; lakini mkuu mmoja ataikomesha aibu iliyoletwa na yeye; naam, aibu yake hiyo atamrudishia mwenyewe. 19#Zab 37:36 Ndipo atauelekeza uso wake kwenye ngome za nchi yake mwenyewe; lakini atajikwaa na kuanguka, wala hataonekana tena. 20Ndipo badala yake atasimama mmoja, atakayepitisha mwenye kutoza ushuru kati ya utukufu wa ufalme wake; lakini katika muda wa siku chache ataangamizwa, si kwa hasira, wala si katika vita.
21 #
1 Sam 3:13; 2 Sam 15:6 Kisha badala yake atasimama mmoja, mtu astahiliye kudharauliwa, ambaye hawakumpa heshima ya ufalme; naye atakuja wakati wa amani, naye ataupata ufalme kwa kujipendekeza. 22#Dan 8:10,24 Na wale wenye silaha mfano wa gharika watagharikishwa mbele yake, na kuvunjika, naam, mkuu wa maagano pia. 23Na baada ya maagano atatenda kwa hila; maana atapanda, naye atakuwa hodari pamoja na watu wadogo. 24Wakati wa amani atapaingia mahali palipofanikiwa sana pa mkoa huo; naye atatenda mambo ambayo baba zake hawakuyatenda, wala babu zake; atatawanya kati yao mawindo, na mateka, na mali; naam, atatunga hila zake juu ya ngome, hata wakati ulioamriwa. 25Naye atachochea nguvu zake na ushujaa wake juu ya huyo mfalme wa kusini kwa jeshi kubwa; na mfalme wa kusini atafanya vita kwa jeshi kubwa mno lenye nguvu nyingi; lakini hatafanikiwa; maana watamfanyia njama. 26#Mik 7:5 Naam, walao sehemu ya chakula chake watavunja jeshi lake na kuliteka mbali na wengi watauwawa kwa kuchinjwa. 27#Zab 12:2 Na katika habari za wafalme hao wawili, mioyo yao watanuia kutenda madhara, nao watasema uongo walipo pamoja mezani; lakini hilo halitafanikiwa; maana mwisho utatokea wakati ulioamriwa. 28Ndipo atakaporudi mpaka nchi yake mwenye utajiri mwingi; na moyo wake utakuwa kinyume cha hilo agano takatifu; naye atafanya kama apendavyo, na kurudi mpaka nchi yake. 29Kwa wakati ulioamriwa atarudi, na kuingia upande wa kusini; lakini wakati wa mwisho mambo hayatakuwa kama yalivyokuwa wakati wa kwanza. 30#Hes 24:24; Yer 2:10 Maana merikebu za Kitimu zitakuja kupigana naye; basi atavunjika moyo, naye atarudi na kulighadhibikia hilo agano takatifu; na kutenda kadiri apendavyo; naam, atarudi, na kuwasikiliza walioacha hilo agano takatifu. 31#Dan 9:27; 8:11; 12:11; Mt 24:15; Mk 13:14 Na wenye silaha watasimama upande wake, nao watapatia unajisi mahali patakatifu, ndiyo ngome, nao wataondoa sadaka ya kuteketezwa ya kila siku, nao watalisimamisha chukizo la uharibifu. 32#1 Nya 28:9 Na wao wafanyao maovu juu ya hilo agano atawapotosha kwa maneno ya kujipendekeza; lakini watu wamjuao Mungu wao watakuwa hodari, na kutenda mambo makuu. 33#Mal 2:7; Ebr 11:35 Na hao wenye hekima katika watu watafundisha wengi; hata hivyo wataanguka kwa upanga, na kwa moto, na kwa kufungwa, na kwa kutekwa nyara, siku nyingi. 34Basi watakapoanguka, watasaidiwa kwa msaada kidogo; lakini wengi wataambatana nao kwa maneno ya kujipendekeza. 35Na baadhi yao wenye hekima wataanguka, ili kuwatakasa, na kuwasafisha, na kuwafanya weupe, hata wakati wa mwisho; kwa maana ni kwa wakati ulioamriwa, ambao haujaja. 36#2 The 2:3-4; Ufu 13:5-6 Naye mfalme atafanya kama apendavyo; naye atajitukuza na kujiadhimisha juu ya kila mungu, naye atanena maneno ya ajabu juu ya Mungu wa miungu, naye atafanikiwa mpaka ghadhabu itakapotimia; maana yaliyokusudiwa yatafanyika. 37#Isa 14:13 Wala hataijali miungu ya baba zake; wala yeye aliyetamaniwa na wanawake; wala hatamjali mungu awaye yote; maana atajitukuza mwenyewe juu ya wote. 38Lakini katika mahali pake atamheshimu mungu wa ngome; na mungu ambaye baba zake hawakumjua atamheshimu, kwa dhahabu, na fedha, na vito vya thamani, na vitu vipendezavyo. 39Naye ataziteka nyara ngome zenye nguvu kwa msaada wa mungu mgeni; na yeye atakayemkubali atamwongeza kwa utukufu; naye atawapa kumiliki wengi; naye ataigawa nchi kwa rushwa.
Wakati wa mwisho
40Na wakati wa mwisho mfalme wa kusini atashindana naye; na mfalme wa kaskazini atamshambulia kama upepo wa kisulisuli, pamoja na magari ya vita, na wapanda farasi, na merikebu nyingi; naye ataingia katika nchi hizo, na kufurika na kupita katikati. 41Tena ataingia katika hiyo nchi ya uzuri, na nchi nyingi zitapinduliwa; lakini nchi hizi zitaokolewa na mkono wake, Edomu, na Moabu, na wakuu wa watu wa Amoni. 42Naye ataunyosha mkono wake juu ya nchi hizo, hata na nchi ya Misri haitaokoka. 43Lakini atakuwa na nguvu juu ya hazina za dhahabu na fedha, na juu ya vitu vyote vya Misri vyenye thamani; na Walibya na Wakushi watafuata nyayo zake. 44Lakini habari zitokazo mashariki na kaskazini zitamfadhaisha; naye atatoka kwa ghadhabu nyingi, ili kuharibu, na kuwaondolea mbali watu wengi. 45#Zab 48:2 Naye ataweka hema zake za kifalme kati ya bahari na mlima mtakatifu wa uzuri; lakini ataifikia ajali yake, wala hakuna atakayemsaidia.
Iliyochaguliwa sasa
Danieli 11: SRUV
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.