Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 9:1-19

Matendo 9:1-19 SRUV

Lakini Sauli, akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu, akataka ampe barua za kuenda Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa Njia hii, wanaume kwa wanawake, awafunge na kuwaleta Yerusalemu. Wakati alipokuwa akisafiri, ikawa anakaribia Dameski; ghafla nuru kutoka mbinguni ikamwangaza kotekote. Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona wanitesa? Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayemtesa. Lakini simama, uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda. Na wale watu waliosafiri pamoja naye wakasimama kimya, waliisikia sauti, lakini hawakuona mtu. Sauli akainuka katika nchi, na macho yake yalipofumbuka, hakuona kitu; wakamshika mkono wakamleta mpaka Dameski. Akawa siku tatu haoni; hali, wala hanywi. Basi palikuwapo Dameski mwanafunzi jina lake Anania. Bwana akamwambia katika maono, Anania. Akasema, Mimi hapa, Bwana. Bwana akamwambia, Simama, nenda zako katika njia iitwayo Nyofu, ukaulize katika nyumba ya Yuda mtu aitwaye Sauli, wa Tarso; maana, angalia, anaomba; naye amemwona mtu, jina lake Anania, akiingia, na kumwekea mikono juu yake, apate kuona tena. Lakini Anania akajibu, Bwana, nimesikia habari za mtu huyu kwa watu wengi, mabaya mengi aliyowatenda watakatifu wako Yerusalemu; hata hapa ana amri itokayo kwa wakuu wa makuhani awafunge wote wakuitiao Jina lako. Lakini Bwana akamwambia, Nenda tu; kwa maana huyu ni chombo kiteule kwangu, alichukue Jina langu mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli. Maana nitamwonesha yalivyo mengi yatakayompasa kuteswa kwa ajili ya Jina langu. Anania akaenda zake, akaingia mle nyumbani; akamwekea mikono akisema, Ndugu Sauli, Bwana amenituma, Yesu, yeye aliyekutokea katika njia uliyoijia, upate kuona tena, ukajazwe Roho Mtakatifu. Mara vikaanguka machoni pake vitu kama magamba, akapata kuona, akasimama, akabatizwa; akala chakula, na kupata nguvu.

Soma Matendo 9

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Matendo 9:1-19