Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 7:1-16

Matendo 7:1-16 SRUV

Kuhani Mkuu akasema, Je! Mambo hayo ndivyo yalivyo? Naye akasema, Ndugu zangu na baba zangu, sikilizeni: Mungu wa utukufu alimtokea baba yetu Abrahamu, alipokuwa katika Mesopotamia, kabla hajakaa Harani, akamwambia, Toka katika nchi yako na katika jamaa zako, ukaende hata nchi nitakayokuonesha. Ndipo alipotoka katika nchi ya Wakaldayo, akakaa Harani, akatoka huko baada ya kufa babaye, Mungu akamhamisha mpaka nchi hii mnayokaa ninyi sasa. Wala hakumpa urithi humu hata kiasi cha kuweka mguu; akaahidi kwamba atampa, iwe milki yake, na ya uzao wake baadaye alipokuwa hana mtoto. Mungu akanena hivi, ya kwamba wazawa wake watakuwa wageni katika nchi ya watu wengine, nao watawafanya kuwa watumwa wao, na kuwatenda mabaya kwa muda wa miaka mia nne. Na lile taifa watakaowafanya watumwa nitawahukumu mimi, alisema Mungu; na baada ya hayo watatoka, nao wataniabudu mahali hapa. Akampa agano la tohara; basi Abrahamu akamzaa Isaka, akamtahiri siku ya nane. Isaka akamzaa Yakobo. Yakobo akawazaa wale kumi na wawili, wazee wetu. Wale wazee wetu wakimwonea wivu Yusufu, wakamwuza aende Misri. Mungu akawa pamoja naye, akamtoa katika dhiki zake zote, akampa fadhili na hekima mbele ya Farao, mfalme wa Misri; naye akamfanya awe mtawala juu ya Misri na nyumba yake yote. Basi kukawa na njaa katika nchi yote ya Misri na Kanaani, na dhiki nyingi, wala baba zetu hawakupata chakula cha kuwatosha. Hata Yakobo aliposikia ya kwamba huko Misri kuna nafaka, akawatuma baba zetu mara ya kwanza. Hata safari ya pili Yusufu akajitambulisha kwa ndugu zake, jamaa ya Yusufu ikawa dhahiri kwa Farao. Yusufu akatuma watu akamwita Yakobo babaye na jamaa zake wote pia, watu sabini na watano. Basi Yakobo akashuka mpaka Misri; akafa yeye na baba zetu; wakachukuliwa mpaka Shekemu wakazikwa katika kaburi lile, ambalo Abrahamu alilinunua kwa kima fulani cha fedha kutoka kwa wana wa Hamori, huko Shekemu.

Soma Matendo 7