Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 27:1-26

Matendo 27:1-26 SRUV

Basi ilipoamriwa tuabiri hadi Italia, wakamtia Paulo na wafungwa wengine katika mikono ya ofisa mmoja, jina lake Yulio, wa kikosi cha Augusto. Tukapanda katika merikebu ya Adramitio iliyokuwa tayari kusafiri mpaka miji ya pwani za Asia, tukatweka; Aristarko, Mmakedonia wa Thesalonike, akiwa pamoja nasi. Siku iliyofuata tukawasili Sidoni; Yulio akamfadhili sana Paulo akampa ruhusa kwenda kwa rafiki zake, apate kutunzwa. Kutoka huko tukiwa baharini, tukasafiri chini ya Kipro ili kujikinga upepo, kwa maana upepo ulikuwa unatukabili. Tulipopita bahari ya upande wa Kilikia na Pamfilia, tukafika Mira, mji wa Likia. Na huko yule ofisa akakuta merikebu ya Aleksandria, tayari kusafiri kwenda Italia, akatupandisha humo. Tukasafiri polepole kwa muda wa siku nyingi, tukafika mpaka Nido kwa shida; na kwa sababu upepo ulikuwa ukituzuia tukapita chini ya Krete, tukaikabili Salmone. Tukaipita kwa shida, pwani kwa pwani, tukafika mahali paitwapo Bandari Nzuri. Karibu na hapo pana mji uitwao Lasea. Na wakati mwingi ulipokwisha kupita, na safari ikiwa ina hatari sasa, kwa sababu siku za kufunga zilikuwa zimekwisha kupita, Paulo akawaonya, akawaambia, Wanaume, naona kwamba safari hii itakuwa na madhara na hasara nyingi, si ya shehena na merikebu tu, ila na ya maisha yetu pia. Lakini yule ofisa akawasikiliza nahodha na mwenye merikebu zaidi ya yale aliyoyasema Paulo. Na kwa sababu bandari ile ilikuwa haifai kukaa wakati wa baridi, wengi wao wakatoa shauri la kutweka kutoka huko ili wapate kufika Foinike, kama ikiwezekana, na kukaa huko wakati wa baridi; nayo ni bandari ya Krete, inaelekea kaskazini mashariki na kusini mashariki. Na upepo wa kusi ulipoanza kuvuma kidogo, wakidhani ya kuwa wamepata waliyoazimu kupata, wakang'oa nanga, wakasafiri karibu na Krete kandokando ya pwani. Baada ya muda mchache ukavuma upepo wa nguvu wa namna ya tufani, uitwao Eurakilo, merikebu iliposhikwa, na kutoweza kushindana na upepo, tukaiacha tukachukuliwa. Na tukipita upesi karibu na kisiwa kidogo kiitwacho Kauda tukadiriki kuikweza mashua; lakini kwa shida. Walipokwisha kuikweza wakatumia misaada, wakaikaza merikebu kwa kupitisha kamba chini yake, nao wakiogopa wasije wakakwama katika fungu liitwalo Sirti, wakatua matanga wakachukuliwa vivi hivi. Na kwa maana tulikuwa tukipigwa sana na ile tufani, kesho yake wakaanza kuitupa shehena baharini. Siku ya tatu wakatupa vyombo vya merikebu kwa mikono yao wenyewe. Jua wala nyota hazikuonekana kwa muda wa siku nyingi, na tufani kuu ikatushika, basi tukakata tamaa ya kuokoka. Na walipokuwa wamekaa wakati mwingi bila kula chakula, Paulo akasimama katikati yao, akasema, Wanaume, iliwapasa kunisikiliza mimi na kutokung'oa nanga huko Krete, na kupata madhara haya na hasara hii. Sasa nawapeni shauri, iweni na moyo mkuu, kwa maana hapana hata nafsi mmoja miongoni mwenu atakayepotea, ila merikebu tu. Kwa maana usiku huu wa leo malaika wa Mungu yule ambaye mimi ni wake, naye ndiye nimwabuduye, alisimama karibu nami, akaniambia, Usiogope, Paulo, huna budi kusimama mbele ya Kaisari; tena, tazama, Mungu amekupa watu wote wanaosafiri pamoja nawe. Basi, wanaume, changamkeni; kwa sababu namwamini Mungu, ya kwamba yatakuwa vile vile kama nilivyoambiwa. Lakini hatuna budi kupwelewa katika kisiwa kimoja.

Soma Matendo 27

Video for Matendo 27:1-26

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Matendo 27:1-26