Matendo 2:6-21
Matendo 2:6-21 SRUV
Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe. Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya? Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo? Waparthi na Wamedi na Waelami, nao wakaao Mesopotamia, Yudea na Kapadokia, Ponto na Asia, Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libya karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu, Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu. Wakashangaa wote wakaingiwa na shaka, wakiambiana, Maana yake nini mambo haya? Wengine walidhihaki, wakisema, wamelewa kwa mvinyo mpya. Lakini Petro akasimama pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti yake, akawaambia, Enyi watu wa Yudea, na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, lijueni jambo hili, mkasikilize maneno yangu. Sivyo mnavyodhani; watu hawa hawakulewa, kwa maana ni saa tatu ya mchana; lakini jambo hili ni lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Yoeli, Itakuwa siku za mwisho, asema Mungu, nitawamwagia watu wote Roho yangu, na wana wenu na binti zenu watatabiri; na vijana wenu wataona maono; na wazee wenu wataota ndoto. Naam, na siku zile nitawamwagia watumishi wangu wanaume na wanawake Roho yangu, nao watatabiri. Nami nitatoa ajabu katika mbingu juu, na ishara katika nchi chini, damu na moto, na mvuke wa moshi. Jua litageuka kuwa giza, na mwezi kuwa damu, kabla ya kuja ile siku ya Bwana iliyo kuu na iliyo dhahiri. Na itakuwa kila atakayeliitia jina la Bwana ataokolewa.