Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 18:1-22

Matendo 18:1-22 SRUV

Baada ya mambo hayo, Paulo akatoka Athene akafika Korintho. Akamwona Myahudi mmoja, jina lake Akila, mzalia wa Ponto; naye amekuja kutoka nchi ya Italia siku za karibu, pamoja na Priskila mkewe, kwa sababu Klaudio amewaamuru Wayahudi wote watoke Rumi, naye akafika kwao; na kwa kuwa kazi yao ya ufundi ilikuwa moja, akakaa kwao, wakafanya kazi pamoja, kwa maana walikuwa mafundi wa kushona hema. Akatoa hoja zake katika sinagogi kila sabato, akajaribu kuwavuta Wayahudi na Wagiriki. Hata Sila na Timotheo walipoteremka kutoka Makedonia, Paulo akasongwa sana na lile neno, akiwashuhudia Wayahudi ya kwamba Yesu ni Kristo. Walipopingana naye na kumtukana Mungu, akakung'uta mavazi yake, akawaambia, Damu yenu na iwe juu ya vichwa vyenu; mimi ni safi; tangu sasa nitakwenda kwa watu wa Mataifa. Akaondoka huko akaingia katika nyumba ya mtu mmoja jina lake Tito Yusto, mcha Mungu, ambaye nyumba yake ilikuwa mpaka mmoja na sinagogi. Na Krispo, mkuu wa sinagogi, akamwamini Bwana pamoja na nyumba yake yote. Wakorintho wengi waliposikia, waliamini, wakabatizwa. Bwana akamwambia Paulo kwa maono usiku, Usiogope, bali nena, wala usinyamaze, kwa kuwa mimi ni pamoja nawe, wala hapana mtu atakayekushambulia ili kukudhuru; kwa maana mimi nina watu wengi katika mji huu. Akakaa huko muda wa mwaka mmoja na miezi sita akifundisha kati yao neno la Mungu. Hata Galio alipokuwa mtawala wa Akaya, Wayahudi wakamwinukia Paulo kwa nia moja, wakamleta mbele ya kiti cha hukumu, wakisema Mtu huyu huwashawishi watu ili wamwabudu Mungu kinyume cha sheria. Na Paulo alipotaka kufunua kinywa chake, Galio akawaambia Wayahudi, Kama lingekuwa jambo la dhuluma au la hila mbaya, enyi Wayahudi, ingekuwa haki mimi kuchukuliana nanyi; bali ikiwa ni hoja juu ya maneno na majina na sheria yenu, liangalieni ninyi wenyewe, maana mimi sitaki kuwa mwamuzi wa mambo hayo. Akawafukuza waondoke mbele ya kiti cha hukumu. Nao wote wakamshika Sosthene, mkuu wa sinagogi, wakampiga mbele ya kiti cha hukumu. Wala Galio hakuyaona mambo hayo kuwa ni kitu. Baada ya hayo Paulo akazidi kukaa huko siku nyingi, kisha akaagana na ndugu akaabiri kwenda Shamu; na Priskila na Akila wakaenda pamoja naye, alipokwisha kunyoa kichwa chake huko Kenkrea; maana alikuwa ana nadhiri. Wakafika Efeso, akawaacha huko. Yeye mwenyewe akaingia katika sinagogi, akahojiana na Wayahudi. Walipomtaka akae muda mrefu zaidi, hakukubali; bali aliagana nao, akisema, Nitarejea kwenu tena, Mungu akinijalia. Akatweka, akatoka Efeso, na alipokwisha kushuka Kaisaria, akapanda juu, akawasalimu kanisa, kisha akateremka kwenda Antiokia.

Soma Matendo 18

Video for Matendo 18:1-22

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Matendo 18:1-22