Matendo 17:13-34
Matendo 17:13-34 SRUV
Lakini Wayahudi wa Thesalonike walipopata habari ya kwamba neno la Mungu linahubiriwa na Paulo hata katika Beroya, wakaenda huko nako wakawavuruga na kuwafadhaisha makutano. Mara hiyo wale ndugu wakamtuma Paulo aende zake mpaka pwani; bali Sila na Timotheo wakabakia huko. Lakini wale waliomsindikiza Paulo wakampeleka mpaka Athene; nao wakiisha kupokea maagizo kuwapelekea Sila na Timotheo, ya kwamba wasikawie kumfuata, wakaenda zao. Paulo alipokuwa akiwangojea huko Athene na kuona jinsi mji ule ulivyojaa sanamu, roho yake ilichukizwa sana ndani yake. Basi katika sinagogi akahojiana na Wayahudi na waliomcha Mungu, na wale waliokutana naye sokoni kila siku. Na baadhi ya Waepikureo na Wastoiko, wenye ujuzi, wakakutana naye. Wengine wakasema, Mpuzi huyu anataka kusema nini? Wengine walisema, Anaonekana kuwa mtangaza habari za miungu migeni, kwa maana alikuwa akihubiri habari za Yesu na ufufuo. Wakamshika, wakampeleka Areopago, wakisema, Je! Twaweza kujua maana ya elimu hii mpya unayoinena? Kwa maana unaleta mambo mageni masikioni mwetu, tutapenda kujua, basi, maana ya mambo haya. Kwa maana Waathene na wageni waliokaa huko walikuwa hawana nafasi kwa jambo linginelo isipokuwa kuelezea au kusikiliza habari za jambo jipya. Paulo akasimama katikati ya Areopago, akasema, Enyi watu wa Athene, katika mambo yote naona ya kuwa ninyi ni watu wa kutafakari sana mambo ya dini. Kwa sababu nilipokuwa nikipita huku na huko na kuyaona mambo ya ibada yenu, niliona madhabahu iliyoandikwa maneno haya, KWA MUNGU ASIYEJULIKANA. Basi mimi nawahubirini habari zake yeye ambaye ninyi mnamwabudu bila kumjua. Mungu aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika hekalu zilizojengwa kwa mikono; wala hatumikiwi kwa mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji kitu chochote; kwa maana ndiye anayewapa wote uzima na pumzi na vitu vyote. Naye alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao; ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasapapasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu. Kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu. Kama vile mmoja wenu, mtunga mashairi alivyosema, Maana sisi sote tu wazawa wake. Basi, kwa kuwa sisi tu wazawa wa Mungu, haitupasi kudhani ya kuwa Uungu ni mfano wa dhahabu au fedha au jiwe, vitu vilivyochongwa kwa ustadi na akili za wanadamu. Basi, zamani zile za ujinga Mungu alijifanya kama hazioni; bali sasa anawaagiza watu wote wa kila mahali watubu. Kwa maana ameweka siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule aliyemchagua; naye amewapa watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu. Basi waliposikia habari za ufufuo wa wafu wengine walifanya dhihaka; wengine wakasema, Tutakusikiliza tena kuhusu habari hiyo. Basi hivi Paulo akaondoka akawaacha. Baadhi ya watu wakaungana naye, wakaamini; katika hao alikuwamo Dionisio, Mwareopago, na mwanamke mmoja jina lake Damari, na watu wengine pamoja na hao.