Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 16:1-15

Matendo 16:1-15 SRUV

Basi akafika Derbe na Listra, na hapo palikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Timotheo, mwana wa mwanamke Myahudi aliyeamini; lakini babaye alikuwa Mgiriki. Mtu huyo alishuhudiwa vema na ndugu waliokaa Listra na Ikonio. Paulo akamtaka huyo afuatane naye, akamtwaa akamtahiri kwa ajili ya Wayahudi waliokuwako pande zile; kwa maana wote walijua ya kuwa babaye ni Mgiriki. Basi walipokuwa wakipita kati ya miji ile, wakawapa zile amri zilizoamriwa na mitume na wazee walioko Yerusalemu, ili wazishike. Makanisa yakatiwa nguvu katika ile Imani, hesabu yao ikaongezeka kila siku. Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile neno katika Asia. Walipofika kukabili Misia wakajaribu kuenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa, wakapita Misia wakateremka kwenda Troa. Paulo akatokewa na maono usiku; alimwona mtu wa Makedonia amesimama, akimsihi, na kumwambia, Vuka, uje Makedonia utusaidie. Basi alipokwisha kuyaona yale maono, mara tukataka kutoka kwenda Makedonia, kwa kuwa tuliona hakika ya kwamba Mungu ametuita tuwahubirie Habari Njema. Basi tukang'oa nanga kutoka Troa, tukafika Samothrake kwa tanga moja, na siku ya pili tukafika Neapoli; na kutoka hapo tukafika Filipi, mji wa Makedonia, mji ulio mkuu katika jimbo lile, mahali walipohamia Warumi; tukawa katika mji huu, tukakaa siku kadhaa. Siku ya sabato tukatoka nje ya lango, tukaenda kando ya mto, ambapo tulidhani ya kuwa pana mahali pa kusali; tukaketi, tukasema na wanawake waliokutana pale. Mwanamke mmoja, jina lake Lidia, mwenye kuuza rangi ya zambarau, mwenyeji wa Thiatira, mcha Mungu, akatusikiliza, ambaye moyo wake ulifunguliwa na Bwana, ayatunze maneno yaliyonenwa na Paulo. Hata alipokwisha kubatizwa, yeye na nyumba yake, akatusihi, akisema, Kama mmeniona kuwa mwaminifu kwa Bwana, ingieni nyumbani mwangu mkakae. Akatusihi sana.

Soma Matendo 16

Video for Matendo 16:1-15