Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 11:1-18

Matendo 11:1-18 SRUV

Basi mitume na ndugu waliokuwako katika Yudea wakapata habari ya kwamba watu wa Mataifa nao wamelipokea neno la Mungu. Na Petro alipopanda kwenda Yerusalemu, wale walio wa tohara wakashindana naye, wakisema, Uliingia kwa watu wasiotahiriwa ukala nao. Petro akaanza kuwaeleza kwa taratibu, akasema, Nilikuwa katika mji wa Yafa, nikiomba, roho yangu ikazimia, nikaona maono; chombo kinashuka, kama nguo kubwa inateremshwa kutoka mbinguni kwa pembe zake nne, kikanifikia. Nikakitazama sana, nikifikiri, nikaona wanyama wa nchi wenye miguu minne, na wanyama wa mwituni, wale watambaao, na ndege wa angani. Nikasikia na sauti ikiniambia, Ondoka, Petro, ukachinje ule. Nikasema, Hasha, Bwana, kwa maana kitu kilicho kichafu au kilicho najisi hakijawahi kuingia kinywani mwangu. Sauti ikanijibu mara ya pili kutoka mbinguni, Alivyovitakasa Mungu, usivinene wewe najisi. Jambo hili likatendeka mara tatu, kisha vitu vyote vikavutwa tena juu mbinguni. Na tazama, mara hiyo watu watatu wakasimama mbele ya nyumba tuliyokuwamo, waliotumwa kwangu kutoka Kaisaria. Roho akaniambia nifuatane nao, nisione tashwishi. Ndugu hawa sita nao wakaenda pamoja nami, tukaingia katika nyumba ya mtu yule; akatueleza jinsi alivyomwona malaika aliyesimama nyumbani mwake na kumwambia, Tuma watu kwenda Yafa ukamwite Simoni aitwaye Petro, atakayekuambia maneno ambayo yatakuokoa, wewe na nyumba yako yote. Ikawa nilipoanza kunena, Roho Mtakatifu akawashukia kama alivyotushukia sisi mwanzo. Nikalikumbuka neno lile la Bwana, jinsi alivyosema, Yohana alibatiza kwa maji kweli, bali ninyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu. Basi ikiwa Mwenyezi Mungu amewapa wao karama ile ile aliyotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo, mimi ni nani niweze kumpinga Mungu? Waliposikia maneno haya wakanyamaza, wakamtukuza Mungu, wakisema, Basi, Mungu amewajalia hata mataifa nao toba liletalo uzima.

Soma Matendo 11