2 Samweli 5
5
Daudi atiwa mafuta kuwa mfalme wa Israeli
1 #
1 Nya 12:23; Mwa 29:14 Ndipo watu wa kabila zote za Israeli wakamwendea Daudi huko Hebroni, wakasema naye, wakinena, Tazama, sisi tu mfupa wako na nyama yako. 2#1 Sam 18:13; 16:1; 2 Sam 7:7; Zab 78:71 Zamani za kale, hapo Sauli alipokuwa mfalme juu yetu, wewe ndiwe uliyewaongoza Israeli wakitoka nje kwenda, na kurudi vitani. Naye BWANA akakuambia, Wewe utawalisha watu wangu Israeli, nawe utakuwa mkuu juu ya Israeli. 3#1 Nya 11:3; 2 Fal 11:17; Amu 11:11; 1 Sam 23:18 Basi wazee wote wa Israeli wakamwendea mfalme huko Hebroni, naye mfalme Daudi akapatana nao huko Hebroni mbele za BWANA; wakamtia Daudi mafuta awe mfalme juu ya Israeli.
4 #
1 Fal 2:11; 1 Nya 3:4; 29:27; 26:31 Daudi alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoanza kutawala, akatawala miaka arubaini. 5Huko Hebroni alitawala miaka saba na miezi sita; na katika Yerusalemu alitawala miaka thelathini na tatu juu ya Israeli wote na Yuda.
Yerusalemu yafanywa makao makuu
6 #
Yos 15:63; Amu 1:21; 19:11 Kisha mfalme na watu wake wakaenda Yerusalemu ili kupigana na Wayebusi, wenyeji wa nchi ile; nao wakamwambia Daudi, hutaingia humu kamwe; maana hata vipofu na viwete watakufukuzia mbali; huku wakidhania ya kuwa Daudi hawezi kuingia humo. 7Lakini Daudi aliiteka ngome ya Sayuni; huu ndio mji wa Daudi. 8#1 Nya 11:6 Naye Daudi alisema siku hiyo, Yeye atakayewapiga Wayebusi, na apande kwenye mfereji wa maji, na kuwapiga viwete, na hao vipofu, ambao roho yake Daudi inawachukia. Kwa sababu hii watu husema, Wako vipofu na viwete hawawezi kuingia nyumbani.#5:8 Maana katika Kiebrania si dhahiri. 9#Amu 9:6,20; 1 Fal 9:24; 11:27; 2 Nya 32:5 Basi Daudi akakaa ndani ya ngome hiyo, akaiita mji wa Daudi. Kisha Daudi akajenga toka Milo na pande za ndani. 10Naye Daudi akazidi kuwa mkuu; kwa maana BWANA, Mungu wa majeshi, alikuwa pamoja naye.
11 #
1 Fal 5:2; 1 Nya 14:1 Kisha Hiramu, mfalme wa Tiro, akatuma wajumbe kwa Daudi, akampelekea na mierezi, na maseremala, na waashi; nao wakamjengea Daudi nyumba. 12#1 Fal 10:9; 2 Nya 2:11; Est 4:14; Isa 45:4 Akajua Daudi ya kwamba BWANA amemweka imara awe mfalme juu ya Israeli, na ufalme wake ameutukuza kwa ajili ya watu wake, Israeli.
13 #
Mwa 25:5,6; Kum 17:17 Naye Daudi akazidi kujitwalia masuria na wake huko Yerusalemu baada ya kutoka Hebroni; wakazaliwa zaidi kwa Daudi wana na binti. 14Na haya ndiyo majina ya hao waliozaliwa kwake huko Yerusalemu; Shamua, na Shobabu, na Nathani, na Sulemani, 15na Ibhari, na Elishua; na Nefegi, na Yafia; 16na Elishama, na Eliada, na Elifeleti.
Shambulizi la Wafilisti lazimwa
17 #
1 Nya 11:16; 2 Sam 23:14 Na hao Wafilisti waliposikia kwamba wamemtia Daudi mafuta ili awe mfalme juu ya Israeli, Wafilisti wote wakapanda kumtafuta Daudi; naye Daudi akapata habari, akashuka akaenda ngomeni. 18#Yos 15:8; Isa 17:5 Basi Wafilisti walikuwa wamekuja na kujitawanya bondeni mwa Warefai. 19#Hes 27:21; Yos 9:14; 1 Sam 23:2,4; 2 Sam 2:1 Basi Daudi akauliza kwa BWANA, akisema, Je! Nipande juu ya Wafilisti? Utawatia mkononi mwangu? Naye BWANA akamwambia Daudi, Panda; kwa kuwa hakika nitawatia Wafilisti mikononi mwako. 20#Isa 28:21 Basi Daudi akaja Baal-perasimu,#5:20 Bwana apitaye katikati (yaani ashindaye). naye Daudi akawapiga huko; akasema, BWANA amewafurikia adui zangu mbele yangu, kama mafuriko ya maji. Basi akapaita mahali pale Baal-perasimu. 21Nao wakaziacha sanamu zao huko, na Daudi na watu wake wakaziondolea mbali.
22Lakini wakapanda hao Wafilisti tena mara ya pili, wakajitawanya bondeni mwa Warefai. 23Naye Daudi alipouliza kwa BWANA, alisema, Usipande; zunguka nyuma yao, ukawajie huko mbele ya miforsadi. 24Kisha itakuwa, hapo utakapoisikia sauti ya kwenda katika vilele vya miforsadi, ndipo nawe ujitahidi; kwa maana ndipo BWANA ametoka mbele yako awapige jeshi la Wafilisti. 25Ndivyo alivyotenda Daudi, vile vile kama BWANA alivyomwagiza; naye akawapiga Wafilisti toka Geba hata ujapo Gezeri.
Iliyochaguliwa sasa
2 Samweli 5: SRUV
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.