2 Samweli 11:1-13
2 Samweli 11:1-13 SRUV
Hata ikawa, mwanzo wa mwaka mpya, wakati watokapo wafalme kwenda vitani, Daudi akamtuma Yoabu, na watumishi wake pamoja naye, na Israeli wote; wakawaangamiza Waamoni, wakauzingira Raba. Lakini Daudi mwenyewe akakaa Yerusalemu. Ikawa wakati wa jioni, Daudi akaondoka kitandani, akatembea juu ya dari la jumba la mfalme; na alipokuwa juu ya dari aliona mwanamke anaoga; naye huyo mwanamke alikuwa mzuri sana, wa kupendeza macho. Naye Daudi akatuma mtu akauliza habari za yule mwanamke. Mtu mmoja akasema, Je! Huyu siye Bathsheba, binti Eliamu, mkewe Uria, Mhiti? Basi Daudi akatuma wajumbe, akamtwaa; naye akaingia kwake; naye akalala naye; (maana yule mwanamke amekwisha kutakasika unajisi wake); kisha akarudi nyumbani kwake. Yule mwanamke akachukua mimba; basi akapeleka habari na kumwambia Daudi, akasema, Ni mja mzito. Ndipo Daudi akapeleka habari kwa Yoabu, akisema, Mtume kwangu Uria, Mhiti. Naye Yoabu akamtuma Uria kwa Daudi. Uria alipomwendea Daudi, Daudi alimwuliza habari za Yoabu, na habari za watu, na habari za vita. Daudi akamwambia Uria, Haya, shuka nyumbani kwako, ukanawe miguu yako. Basi Uria akatoka katika nyumba ya mfalme, na tunu ya vyakula ikamfuata, iliyotoka kwa mfalme. Lakini Uria akalala mlangoni pa nyumba ya mfalme, pamoja na watumishi wote wa bwana wake, wala hakushuka nyumbani kwake. Watu walipomwambia Daudi ya kwamba, Uria hakushuka nyumbani kwake, Daudi akamwambia Uria, Je! Hukutoka safarini? Mbona hukushuka nyumbani kwako? Naye Uria akamwambia Daudi, Sanduku, na Israeli, na Yuda, wanakaa vibandani; na bwana wangu Yoabu, na watumishi wa bwana wangu, wamepiga kambi waziwazi uwandani; nami niende nyumbani kwangu, kula na kunywa, na kulala na mke wangu? Uishivyo, na kama roho yako iishivyo, mimi sitafanya jambo hili. Basi Daudi akamwambia Uria, Ngoja hapa leo tena, na kesho nitakuacha kwenda zako. Basi Uria akakaa Yerusalemu siku ile, na siku ya pili yake. Naye Daudi akamwalika, akala, akanywa mbele yake; naye akamlevya; hadi wakati wa jioni akatoka kwenda kulala kitandani mwake pamoja na watumishi wa bwana wake, lakini hakushuka nyumbani kwake.