Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samweli 11:1-13

2 Samweli 11:1-13 NENO

Katika mwanzo wa mwaka mpya, wakati wafalme hutoka kwenda vitani, Daudi akamtuma Yoabu pamoja na watu wa mfalme na jeshi lote la Israeli. Wakawaangamiza Waamoni na kuuzingira mji wa Raba. Lakini Daudi akabaki Yerusalemu. Ikawa siku moja wakati wa jioni Daudi aliinuka kitandani mwake na kutembeatembea juu ya paa la jumba lake la kifalme. Akiwa kule kwenye paa, akamwona mwanamke akioga. Mwanamke huyo alikuwa mzuri sana wa sura, naye Daudi akatuma mtu mmoja kuuliza habari za huyo mwanamke. Huyo mtu akamwambia Daudi, “Je, huyu si Bathsheba binti Eliamu, naye ni mke wa Uria Mhiti?” Ndipo Daudi akatuma wajumbe kumleta. Huyo mwanamke akaja kwa Daudi, Daudi akakutana naye kimwili. (Huyo mwanamke ndipo tu alikuwa amejitakasa kutoka siku zake za hedhi.) Kisha akarudi nyumbani mwake. Huyo mwanamke akapata mimba akampelekea Daudi ujumbe, kusema, “Mimi ni mjamzito.” Ndipo Daudi akapeleka ujumbe kwa Yoabu, “Unipelekee Uria Mhiti.” Naye Yoabu akamtuma Uria kwa Daudi. Uria alipofika, Daudi akamuuliza habari za Yoabu, hali za askari na vita kwamba inaendeleaje. Kisha Daudi akamwambia Uria, “Teremka nyumbani mwako ukanawe miguu yako.” Basi Uria akatoka jumba la kifalme, tena zawadi zikamfuata kutoka kwa mfalme. Lakini Uria akalala kwenye ingilio la jumba la kifalme pamoja na watumishi wote wa bwana wake, na hakuteremka kwenda nyumbani mwake. Daudi alipoambiwa kwamba, “Uria hakuenda nyumbani,” Daudi akamuuliza, “Je, si ndiyo tu umefika kutoka safari ya mbali? Kwa nini hukuenda nyumbani?” Uria akamwambia Daudi, “Sanduku la Mungu, na Israeli na Yuda wanakaa kwenye mahema, naye bwana wangu Yoabu na watu wa bwana wangu wamepiga kambi mahali pa wazi. Ningewezaje kwenda nyumbani mwangu ili nile, ninywe na kukutana na mke wangu? Hakika kama uishivyo sitafanya jambo kama hilo!” Ndipo Daudi akamwambia, “Kaa hapa siku moja zaidi, nami kesho nitakutuma urudi.” Kwa hiyo Uria akakaa Yerusalemu siku ile na siku iliyofuata. Kwa ukaribisho wa Daudi, Uria akala na kunywa pamoja naye, Daudi akamlevya. Lakini jioni Uria alitoka kwenda kulala juu ya mkeka wake miongoni mwa watumishi wa bwana wake, hakuenda nyumbani.