2 Petro 3:8-18
2 Petro 3:8-18 SRUV
Lakini, wapenzi, msilisahau neno hili, kwamba kwa Bwana siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja. Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyodhani anakawia, bali huwavumilia, maana hapendi mtu yeyote apotee, bali wote wafikie toba. Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwizi; katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea. Basi, kwa kuwa vitu hivi vyote vitafumuliwa hivyo, imewapasa ninyi kuwa watu wa tabia gani katika mwenendo mtakatifu na utauwa, mkiingojea hata ije siku ile ya Mungu, na kuihimiza; ambayo katika hiyo mbingu zitafumuliwa zikiungua, na viumbe vya asili vitateketea na kuyeyuka? Lakini, kama ilivyo ahadi yake, mnatazamia mbingu mpya na nchi mpya, ambayo haki yakaa ndani yake. Kwa hiyo, wapenzi, mnapoyangojea mambo hayo, fanyeni bidii ili mwonekane mkiwa na amani, bila doa wala dosari mbele yake. Nanyi uhesabuni uvumilivu wa Bwana wetu kuwa ni wokovu, kama vile na ndugu yetu mpenzi Paulo alivyowaandikia kwa hekima aliyopewa; akisema juu ya mambo haya kama afanyavyo katika barua zake zote pia, katika barua hizo yamo mambo ambayo ni vigumu kuyaelewa na mambo hayo watu wasio na elimu, wasio imara, huyapotoa, kama vile wapotoavyo Maandiko mengine, na kujiletea maangamizi wao wenyewe. Basi, wapenzi kwa kuwa mmejua hayo, jihadharini msije mkapotoshwa na kosa la hao wahalifu mkaanguka na kuuacha uthabiti wenu. Lakini, kueni katika neema, na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo. Utukufu una yeye sasa na hata milele.