Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 24:1-7

2 Wafalme 24:1-7 SRUV

Katika siku zake akakwea Nebukadneza, mfalme wa Babeli, na Yehoyakimu akawa mtumishi wake muda wa miaka mitatu; kisha, akageuka, akamwasi. Naye BWANA akatuma juu yake vikosi vya Wakaldayo, na vikosi vya Washami, na vikosi vya Wamoabi, na vikosi vya wana wa Amoni, akawatuma juu ya Yuda ili kuiharibu, sawasawa na neno la BWANA alilolinena kwa mkono wa watumishi wake manabii. Hakika kwa amri ya BWANA mambo hayo yalimpata Yuda, ili waondoshwe kutoka machoni pake, kwa sababu ya dhambi zake Manase, kadiri ya yote aliyoyafanya; tena kwa ajili ya damu zisizo na hatia alizozimwaga; kwani aliujaza Yerusalemu damu zisizo na hatia; wala BWANA hakukubali kusamehe. Basi mambo yote ya Yehoyakimu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Yuda? Yehoyakimu akalala na babaze; na mwanawe Yekonia akatawala mahali pake. Basi mfalme wa Misri hakuja tena kutoka nchi yake; kwa kuwa mfalme wa Babeli alikuwa amemnyang'anya nchi, tangu kijito cha Misri mpaka mto wa Frati, yote aliyokuwa nayo mfalme wa Misri.