Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 22:1-13

2 Wafalme 22:1-13 SRUV

Yosia alikuwa na umri wa miaka minane alipoanza kutawala; akatawala miaka thelathini na mmoja katika Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Yedida, binti Adaya wa Bozkathi. Akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA, akaenda katika njia yote ya Daudi baba yake, wala hakugeuka upande wa kulia wala wa kushoto. Ikawa, katika mwaka wa kumi na nane wa mfalme Yosia, mfalme akamtuma Shafani, mwana wa Azalia, mwana wa Meshulamu, mwandishi, nyumbani kwa Bwana, akisema, Nenda kwa Hilkia, kuhani mkuu, ili aihesabu fedha yote inayoletwa nyumbani mwa BWANA, ambayo mabawabu wameipokea kwa watu; tena waitie ile fedha katika mikono ya wafanya kazi wanaoisimamia nyumba ya BWANA; wakapewe wafanya kazi waliomo ndani ya nyumba ya BWANA, ili wapate kupatengeneza mahali palipobomoka ndani ya nyumba; wapewe maseremala, na wajenzi, na waashi; ili kununua miti na mawe yaliyochongwa wapate kuitengeneza nyumba. Lakini hawakuulizwa habari za ile fedha waliyokabidhiwa; maana walitenda kazi kwa uaminifu. Naye Hilkia, kuhani mkuu, akamwambia Shafani, mwandishi, Nimekiona kitabu cha Torati katika nyumba ya BWANA. Hilkia akampa Shafani kile kitabu, naye akakisoma. Shafani mwandishi akamwendea mfalme, akamletea mfalme habari tena, akasema, Watumishi wako wamezitoa zile fedha zilizoonekana ndani ya nyumba, nao wamewakabidhi wafanya kazi wanaoisimamia nyumba ya BWANA. Kisha Shafani mwandishi akamwambia mfalme, akasema, Hilkia kuhani amenipa kitabu. Shafani akakisoma mbele ya mfalme. Ikawa, mfalme alipokwisha kuyasikia maneno ya kitabu hicho cha torati, alirarua nguo zake. Mfalme akamwamuru Hilkia kuhani, na Ahikamu, mwana wa Shafani, na Akbori, mwana wa Mikaya, na Shafani mwandishi, na Asaya, mtumishi wa mfalme akasema, Nendeni, mkamwulize BWANA kwa ajili yangu, na kwa ajili ya watu hawa, na kwa ajili ya Yuda yote, kuhusu maneno ya kitabu hiki kilichoonekana; kwa kuwa hasira ya BWANA ni kubwa aliyotukasirikia, kwa sababu baba zetu hawakuyaangalia maneno ya kitabu hiki, kufanya kama hayo yote tuliyoandikiwa.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na 2 Wafalme 22:1-13