2 Wafalme 17:4-23
2 Wafalme 17:4-23 SRUV
Mfalme wa Ashuru akaona fitina katika huyo Hoshea; kwa maana alikuwa ametuma wajumbe kwa So, mfalme wa Misri, wala hakumletea kodi mfalme wa Ashuru, kama alivyofanya mwaka kwa mwaka; kwa hiyo mfalme wa Ashuru akamfunga, akamtia kifungoni. Ndipo mfalme wa Ashuru akakwea katikati ya nchi yote, akaenda Samaria, akauhusuru miaka mitatu. Katika mwaka wa tisa wa Hoshea, huyo mfalme wa Ashuru akautwaa Samaria, akawahamisha Israeli mpaka Ashuru, akawaweka katika Hala na Habori, karibu na mto wa Gozani, na katika miji ya Wamedi. Yalitukia hayo kwa sababu wana wa Israeli walikuwa wametenda dhambi juu ya BWANA, Mungu wao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri watoke chini ya mkono wa Farao mfalme wa Misri, wakawaacha miungu mingine. Wakaziendea sheria za mataifa, ambao BWANA aliwafukuza mbele ya wana wa Israeli, na sheria za wafalme wa Israeli walizozifanya. Tena, wana wa Israeli wakafanya kwa siri mambo yasiyokuwa mema juu ya BWANA, Mungu wao, wakajijengea mahali pa juu katika miji yao yote, kutoka mnara wa walinzi hata katika miji yenye boma. Wakajisimamishia nguzo na maashera juu ya kila mlima mrefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi; wakafukiza uvumba huko katika kila mahali pa juu, kama mataifa walivyofanya, ambao BWANA aliwafukuza mbele yao; wakaunda mambo mabaya, ili wamkasirishe BWANA; wakatumikia sanamu, ambazo BWANA aliwakataza, akasema, Msitende jambo hili. Pamoja na hayo BWANA aliwashuhudia Israeli, na Yuda, kwa kinywa cha kila nabii, na cha kila mwonaji, akisema, Geukeni, na kuziacha njia zenu mbaya, mkazishike amri zangu na hukumu zangu, sawasawa na ile sheria yote niliyowaamuru baba zenu, nikawapelekea kwa kinywa cha manabii watumishi wangu. Walakini hawakutaka kusikia, bali walifanya shingo zao kuwa ngumu, kama shingo za baba zao, wasiomwamini BWANA, Mungu wao. Wakazikataa sheria zake, na agano lake, alilolifanya na baba zao; na shuhuda zake alizowashuhudia; wakafuata ubatili, wakawa ubatili, nao wakaandamana na mataifa waliowazunguka, ambao BWANA alikuwa amewaagiza, wasitende kwa mfano wao. Wakaziacha amri zote za BWANA, Mungu wao, wajitengenezea sanamu za kusubu, yaani, ndama wawili, wakafanya na Ashera, wakaliabudu jeshi lote la mbinguni, wakamtumikia Baali. Wakawapitisha watoto wao, wa kiume na wa kike, motoni, wakapiga ramli, wakafanya uchawi, wakajiuza wenyewe wapate kufanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, hata kumkasirisha. Kwa hiyo BWANA akawaghadhibikia Israeli sana, akawahamisha mbali na uso wake; wala hapana aliyesalia ila kabila la Yuda peke yake. Hata na watu wa Yuda hawakuyashika maagizo ya BWANA, Mungu wao, lakini walikwenda katika amri za Israeli walizokuwa wamezifanya wenyewe. Basi BWANA akakikataa kizazi chote cha Israeli, akawatesa, na kuwatia katika mikono ya watu wenye kuwateka nyara, hata alipokwisha kuwatupa, watoke machoni pake. Maana aliwatenga mbali Israeli na nyumba ya Daudi; nao wakamfanya Yeroboamu mwana wa Nebati kuwa mfalme; Yeroboamu akawavuta Israeli wasimfuate BWANA, akawakosesha kosa kubwa. Nao wana wa Israeli wakaendelea katika dhambi zote za Yeroboamu alizozifanya; hawakujiepusha nazo; hata BWANA akawaondoa Waisraeli wasiwe mbele zake, kama vile alivyosema kwa kinywa cha watumishi wake wote, manabii. Basi Waisraeli walichukuliwa mateka kutoka nchi yao wenyewe, waende nchi ya Ashuru, hata leo.